Na Thabit Hamidu,Zanzibar.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ),imesema haina mpango wa kuunda sheria itakayozipa mamlaka Serikali za mitaa uwezo wa kutengewa fungu la kusaidia kukamilisha shughuli za ujenzi wa barabara za ndani.
Kauli hiyo ameitoa jana Naibu waziri wa Nchi Ofisi Ofisi ya Raisi ,Tawala za mikoa,Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ Shamata Shaame wakati akijibu swali la Hidaya Ali Makame ambaye ni Mwakilishi wa nafasi za wanawake ambapo alitaka kujua mpango wa serikali katika kuzipa mamlaka hizo za kutengewa fungu la fedha.
Akijibu swali hilo alisema serikali haitaandaa sheria hiyo badala yake itaendelea na utaratibu wake kutoa fursa kwa Halmashauri za Wilaya kupata ruzuku kutoka serikali kwa ajili ya utekelezaji wa mipango yake ikiwemo matengenezo ya barabara za ndani.
Naibu Waziri huyo alisema uwezo wa kutenga fungu hilo utaweza kutekelezwa iwapo fedha zinazotolewa na mfuko wa Barabara zitaengezeka kutoka asilimia 15 inayotolewa sasa hadi kufikia asilimia 40 ya bajeti ya matengenezo ya barabara za ndani hususan vijijini.
Alisema ni kweli kuwa Halmashauri za wilaya zimekuwa vinakabiliwa na tatizo kubwa la matengenezo ya barabara za ndani jambo ambalo linakosesha fursa ya kuzifikia Barabara zote zinazohitaji kutengenezwa.
"Ninachukua fursa hii kuzishauri Halmashauri kudhibiti vyanzo vya mapato ya ndani ili pamoja na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ili fedha zitakazo patikana ziweze kukidhi mahitaji yaliyokusudiwa,"alisema Naibu Waziri huyo.
