Marekani yasema haitaki vita na Iran


Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amesema nchi yake haitaki vita na Iran lakini ameapa wataendelea kuishinikiza Iran.

Kauli hiyo ameitoa wakati akijaribu kutuliza hofu ya jumuia ya kimataifa kuhusu kuongezeka mvutano unaohofiwa unaweza kuzidisha mzozo kati ya Marekani na Iran.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi habari na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, katika mji wa Sochi, Urusi, Pompeo amesema Marekani haitafuti vita na Iran na kwamba Marekani imeweka bayana kwamba iwapo Iran itatishia maslahi ya nchi hiyo, basi kitisho hicho bila shaka kitajibiwa kwa njia inayoeleweka.

''Tunaitaka Iran ifanye mambo yake kama nchi ya kawaida, hilo ndilo tunaloliomba. Tumeweka shinikizo katika uongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ili kulifanikisha hilo. Kimsingi hatutafuti vita na Iran,'' alisema Pompeo.

Pompeo amesema kuwa jana alizungumza na Lavrov na siku ya Jumatatu mjini Brussels, Ubelgiji alizungumza na washirika wake wa Ulaya kuhusu kitisho ambacho Marekani inakiona kutoka kwa Iran.

Matamshi yake yametolewa baada ya Marekani kupeleka manowari ya kubeba ndege za kivita pamoja na ndege za mashambulizi aina ya B-52 katika eneo la Mashariki ya Kati, ingawa Rais Donald Trump amekanusha taarifa kwamba anafikiria kuwapeleka wanajeshi 120,000.

Akizungumza na DW mjini Brussels, mjumbe wa Marekani kwa ajili ya Iran, Brian Hook amesema Ulaya ina dhamana ya kuhakikisha kuwa eneo la Mashariki ya Kati lina amani na utulivu.