TAGCO na Idara ya Habari- MAELEZO zawezesha utatuzi wa changamoto Kada ya Mawasiliano


Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini wa Taasisi na Mashirika ya Umma  Jijini Dodoma wamekipongeza Chama Cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini TAGCO kwa kushirikiana na Idara ya Habari MAELEZO kwa kuendelea kusimamia vyema kada ya Mawasiliano Serikalini.


Wakizungumza wakati wa ziara  ya ujumbe wa Chama hicho na Idara ya Habari  MAELEZO  kutembelea na kujionea changamoto zinazowakabili  ili kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili, Maafisa hao akiwemo Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Ntambi Bunyanzu amesema kuwa utaratibu huo unapaswa kuendelezwa ili kusaidia kuimarisha utendaji wa vitengo vya mawasiliano Serikalini.

“Utaratibu huu  wa kutembelea vitengo vya mawasiliano Serikalini unatoa fursa ya kubaini changamoto zinazokabili vitengo vya mawasiliano serikalini katika Taasisi zetu na unawezwesha kupatikana kwa suluhisho la changamoto hizo hivyo tunaomba uendelezwe” Alisisitiza Bunyanzu.

Akifafanua amesema kuwa amefarijika kuona kuwa utaratibu wa kutembelea Vitengo hivyo umekuwa endelevu na kwa kipindi hiki utasaidia kuendelea kuimarisha mawasiliano Serikalini kama ilivyo azma ya Serikali.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dodoma Bw.  Sebastian Warioba amesema kuwa vitengo hivyo vina jukumu kubwa katika kuimarisha mawasiliano Serikalini ili hatimeye wananchi waweze kufahamu yale yote yanaytotekelezwa na Serikali.

“Tunalo jukumu kubwa la kuendelea kuimarisha mawasiliano serikalini kama Maafisa habari  na Mawasiliano Serikalini hivyo nawahamasisha  wenzangu tuendelee kujituma na kushirikiana na viongozi wetu katika kutoa taarifa kwa umma kuhusu miradi ya maendeleo.” Alisisitiza Warioba

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini (TAGCO) Bi Sarah Kibonde amesema kuwa maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini wanapaswa kufanya kazi kimkakati na kuepuka mazoea.

“Tunalo jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa tunatangaza mafanikio ya Serikali hasa miradi mikubwa ya kimakakati inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano inayolenga kuwaletea wananchi maendeleo,” Alisisitiza

Akifafanua amesema kuwa Chama hicho kwa kushirikiana na Idara ya Habari MAELEZO wataendelea kufanya ufuatiliaji wa utendaji wa maafisa Habari Serikalini ili kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao kwa weledi.

Ziara ya Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini na Idara ya Habari MAELEZO imeanza June 24 , 2019  na inatarajiwa kukamilika June 29, 219 ikishirikisha Taasisi  na Mashirika ya Umma yaliyopo Jijini Dodoma, Baadhi ya Taasisi za zilizotembelewa ni pamoja  DUWASA, Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA).