Huu uhalifu katika ziwa Victoria utashughulikiwa - Waziri Lugola


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amezungumzia uhalifu katika ziwa Victoria, akiwataka Polisi waongeze kasi kwa kufanya operesheni za mara kwa mara katika maeneo hayo ya ziwa kwa lengo la kudhibiti uhalifu huo.

Lugola ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara alipokuwa anazungumza na wananchi wa Mji wa Kibara, Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, leo.

"Huu uhalifu katika ziwa Victoria utashughulikiwa, hii ni awamu ya tano ambayo inaongozwa na Rais Dkt John Magufuli, hivyo tunataka wananchi muishi katika nchi yenu kwa amani na utulivu,” alisema Lugola.

Waziri Lugola anaendelea na ziara jimboni kwake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kufanya mikutano ya hadhara akisikiliza kero za wananchi jimboni humo, na pia kuiongoza ligi yake, Kangi Bomba ambayo inashirikisha wananchi jimboni humo kufanya mashindano ya mpira wa miguu, pete, pamoja na michezo mbalimbali.