Na John Walter-Manyara
Hatimaye kazi ya ukarabati wa taa za barabarani zilizokuwa haziwaki katika Mji wa Babati imeanza kutekelezwa kufuatia agizo la Mkuu wa Mkoa wa Manyara Region kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Kwa muda mrefu baadhi ya wakazi wa Babati walilalamikia
tatizo la taa za barabarani kuzimika hali iliyokuwa ikisababisha hofu ya
usalama nyakati za usiku.
Kufuatia malalamiko hayo, Mkuu wa Mkoa kupitia kikao cha
bodi ya Barabara mkoa kilichofanyika hivi karibuni, aliiagiza TARURA
kuhakikisha taa zote zilizokuwa haziwaki zinarejeshwa katika hali ya kufanya
kazi haraka iwezekanavyo.
Kupitia jukwaa la mitandao la Manyara Mpya, Mkuu
huyo wa Mkoa amethibitisha kuanza kwa utekelezaji wa agizo hilo kwa kuchapisha
picha zinazoonesha mafundi wakiendelea na kazi ya matengenezo ya miundombinu ya
taa hizo.
Akiandika katika ujumbe wake, amesema:
“Ndugu viongozi mliopo mitaani huko Naimani mnaona kazi
inaendelea, taa zilizozima ni nyingi na kazi yote itakamilika, tuwe na subra
tu. Nawashukuru kwa uvumilivu.
Naimani kwenye hili kikombe kimeniepuka 🙇🏽♀️
Nawapenda sana ❤️”
Kauli hiyo imepokelewa kwa hisia chanya na wananchi
wengi, wakionesha matumaini kuwa kukamilika kwa kazi hiyo kutaimarisha usalama,
kuongeza mwanga katika maeneo ya biashara pamoja na kurahisisha shughuli za
kijamii nyakati za usiku.
Utekelezaji huo unaonekana kuwa sehemu ya juhudi za
uongozi wa mkoa katika kusimamia na kuboresha miundombinu ya huduma za kijamii
ndani ya Manispaa ya Babati.


0 Maoni