Serikali kushirikiana na Sekta binafsi kukuza ujuzi wa vijana wahitimu wa vyuo vya Elimu ya juu katika la TEHAMA

Serikali ya awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Mh Rais Dr John Magufuli imesema  itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kukuza ujuzi kwa vijana wahitimu wa Vyuo vikuu na vyuo vya Elimu ya Juu katika eneo la Teknolojia,Habari na Mawasiliano ili kuijengea uwezo wa nguvu kazi ya Nchi kushiriki katika uchumi wa Viwanda kikamilifu.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana na Ajira Mh Anthony Mavunde wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Wahandisi wa TEHAMA iliyoenda sambamba na usaili wa wanachuo kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo ambapo jumla ya wanachuo ishirini wa masomo ya Uhandisi wa TEHAMA watapata nafasi ya kupata mafunzo katika Kampuni mbalimbali nchini.

"Serikali inatekeleza mkakati wa Kukuza Ujuzi  nchini kupitia mafunzo kwa vitendo sehemu za kazi ambapo wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu watapata nafasi ya kuwepo sehemu za kazi kwenye Makampuni na Viwanda kwa miezi 6 mpaka 12, tunashirikiana na sekta binafsi chini ya mwavuli wa TPSF kuhakikisha kwamba waajiri wanatenga nafasi za mafunzo ya vitendo," amesema Mavunde.

Akizungumza kwa niaba ya Vyuo vya Elimu ya Juu Nchini,Dr Mussa Kissaka ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya TEHAMA Chuo Kikuu Dar es salaam (UDSM) ameishukuru Kampuni ya HUAWEI kwa kuwajengea uwezo  wanachuo wahandisi wa TEHAMA na hivyo kuwafanya kuwa na sifa na uwezo wa kuajirika katika soko la ushindani wa Ajira.

Akitoa maelezo ya Utangulizi,Kaimu Meneja Mkuu wa Huawei Tanzania Juck Wang ameeleza kwamba ni dhamira ya Kampuni kushirikiana na Serikali kuwajengea uwezo wahandisi wa TEHAMA Tanzania kuendana na mahitaji ya dunia ya leo na kuahidi kuendelea kuwapeleka wahandisi wengi zaidi wa Kitanzania kwenda nchini China kupata mafunzo ya ziada juu ya teknolojia mbalimbali.