Rais Trump aendeleza kauli za kuwaponda wabunge wanne

Rais Donald Trump ameanza kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2020 na mbinu anayoitumia ni malumbano yaliyopo kati yake na wabunge wanne wanawake wa jamii za walio wachache nchini Marekani ambao ni wakosoaji wake wakubwa.

Rais huyo wa Marekani amesema vitendo vya wabunge hao ndio vinatoa sura halisi ya chama cha Demokratic.

Yote hayo yanatokea baada ya bunge kutoa tamko la kulaani matamshi ya Trump na kusema kwamba ni ya kibaguzi.

Licha ya bunge linalodhibitiwa na chama cha Democtarts kulaani maneno na maoni yake kuhusu wabunge wanne wanawake wa jamii za walio wachache nchini Marekani na kuiita kauli yake kuwa ni ya kibaguzi, Trump alitumia dakika 20 kwenye hotuba yake ya dakika 90 katika jimbo la North Carolina kuwaponda wabunge hao kwa kusema ni kikosi cha watu wenye msimamo mkali wanaoipinga Marekani na ambao wanaichukia Israeli.

Trump pia aliendeleza mashambulio yake dhidi ya wabunge hao kwa kusema wanataka kuijaza Marekani na wahamiaji zaidi.