Maofisa ardhi watakaoshindwa kuingiza miliki za ardhi kwenye mfumo kuchukuliwa hatua


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angeline Mabula amewataka Maafisa ardhi nchini kuhakikisha wanaingiza taarifa za miliki za ardhi kwenye Mifumo ya Utunzaji na Ukadiriaji Kodi za Ardhi kufikia mwezi Oktoba 2019 na watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo watachukuliwa hatua.

Dkt. Mabula alitoa kauli hiyo wilayani Urambo wakati akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi katika wilaya hiyo ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake katika mkoa wa Tabora ambapo alitembelea pia wilaya ya Kaliua kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi sambamba na kukagua masijala za ardhi na mfumo wa ukusanyaji kodi ya Pango la ardhi.

Alisema, Mfumo wa Utunzaji na Ukadiriaji Kodi za Ardhi unasaidia kujua wamiliki wa ardhi na madeni yao kwa urahisi kwa kuwa taarifa kuhusiana na miliki za ardhi sambamba na kiasi wanachodaiwa kinajulikana kwa urahisi hivyo kuiwezesha wizara kuwa na kumbukumbu zilizo na uhakika. ‘’ Wasiotimiza asilimia mia moja inapokwisha mwezi oktoba 2019 nitaanza kushughulika na maafisa ardhi wasioingiza taarifa za miliki za ardhi katika mfumo, kama ni Mteule au Mkuu wa Idara utaondolewa’’ Alisema Dkt Mabula

Kauli ya Dkt. Mabula inafuatia kutoridhishwa na kasi ya uingizaji taarifa za miliki za ardhi katika Mifumo ya Utunzaji na Ukadiriaji Kodi ya Ardhi kwa baadhi ya halmashauri alioueleza kuwa unachangiwa na Maafisa ardhi wasiofanya kazi ipasavyo na kutolea mfano wa halmashauri za Kaliua na Urambo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya Urambo, Joel Mayunga alieleza halmashauri hiyo kuingiza viwanja 3,501 katika mfumo kati ya 4,831 huku Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Abel Busalama akieleza halmashauri ya wilaya yake  kuingiza viwanja 553 kati ya 1,597.