Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wanunuzi wa zao la Pamba katika maeneo mbalimbali nchini wahakikishe wanaongeza kasi ya ununuzi wa zao hilo ili wakulima waweze kupata fedha zao kwa wakati.
Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga pamoja na Manaibu Waziri wake kubaki katika mikoa yote inayolima zao la pamba hadi wakulima wote watakapolipwa fedha zao na kuhakikisha pamba yote iliyomo mikononi mwa wakulima inauzwa.
Ameyasema hayo leo Alhamisi, Agosti 8, 2019 wakati alipotembelea Chama cha Msingi cha Itemelo kilichoko eneo la Dutwa wilayani Bariadi, Simiyu kwa ajili ya kujionea mauzo ya zao la pamba.
Waziri Mkuu amesema ataendelea kusimamia mwenendo wa zao hilo kwa ukaribu lengo likiwa kuona wakulima wananufaika kwa kupata tija. “Ilani ya CCM ya 2015/2020 inasisitiza kilimo na inataka wakulima wapate masoko ya uhakika na tunalitekeleza jambo hilo na pamba yote itanunuliwa.”
Amesema Serikali inataka kuona pamba yote iliyoko kwa wakulima inatoka ili wakulima waweze kulipwa fedha ambazo zitawawezesha kujikimu kimaisha pamoja na kununua pembejeo kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa AMCOS wahakikishe wanawatambua wakulima kwa majina, maeneo wanayoishi pamoja na ukubwa wa mashamba yao ili waweze kuagiza pembejeo kulingana na mahitaji halisi.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewasihi wakulima kufungua akaunti katika taasisi mbalimbali za kifedha lengo likiwa ni kuhifadhi vizuri fedha wanazozipata kutokana na mauzo ya pamba ili ziweze kuwasaidia baadaye.
Pia, Waziri Mkuu amewasisitiza wakulima hao waendelee kutunza vizuri pamba yao na kuipeleka ghalani ikiwa katika hali nzuri ya usafi na ubora wa hali ya juu, kwani kwa sasa pamba ya Tanzania inasifika kwa ubora katika soko la dunia.
Kwa upande wa masoko hususan ya pamba, Waziri Mkuu aliwasisitizia wananchi wa Dutwa na Watanzania kwa ujumla kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli inaendelea kuhakikisha uwepo wa masoko ya uhakika wa mazao yote hususan yale ya kimkakati.
Pia, Waziri Mkuu ameongeza kuwa moja ya agenda muhimu ya ziara yake ya Kiserikali aliyoifanya nchini Misri mwezi Julai 2019 ilikuwa ni kutafuta masoko ya uhakika ya mazao ya Tanzania likiwemo na zao la pamba.

