Shahidi wa Sita kumzamisha Zitto?

ZITTO Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, anayetuhumiwa na tuhuma za uchochezi, kesho shahidi wa sita anatarajiwa kutoa ushahidi dhidi yake. Anaandika Faki Sosi … (endelea).

Shahidi huyo atatoa ushahidi wake kesho tarehe 13 Agosti 2019 pale Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini atakapopanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusikiliza ushahidi huo.

Zitto anatuhumiwa kutoa maneno ya uchochezi kuhusu mauaji yaliyotokea Nguruka, Kigoma. Kesi hiyo ipo katika hatua ya usikilizwaji ambapo upande wa Jamhuri umefikisha shahidi wake wa tano Dk. Ernest Nsumila ambaye aliyetoa ushahidi wake tarehe 16 Julai 2019.

Upande wa utetezi unaongozwa na wakili Peter Kibatala, Dickson Matata na Steven Mwakibolwa ambapo upande wa Jamhuri unawakilishwa na wakili wa serikali mwandamizi Nassoro Katuga.

Huruma Shahidi, ndiye Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo ambapo inatarajiwa upande wa Jamhuri kumpeleka shahidi wa sita.

Dk. Nsumila katika ushahidi wake, alieleza kuwa yeye ni daktari katika kituo cha afya Nguruka, wilayani Nguruka, Kigoma ambapo aliwatibu  majeruhi watatu wanaodaiwa kuwaua askari polisi wawili.

Akiongozwa na wakili Katuga ambapo, Dk Nsumila alidai tarehe 18, Oktoba 2018 akiwa kituo hapo alipokea majeruhi watatu wote wakiwa ni wanaume.

“Nilikuwepo kazini tangu asubuhi, ilipofika  saa 12 jioni nilipokea majeruhi watatu, wote wanaume wanaotokea Kijiji cha Mpeta wakidai wamepigwa risasi na askari polisi kwa madai kuwa, walivamia maeneo ambayo hayatakiwi  kufanya kilimo,” alidai.

Alieleza kuwa, majeruhi hao walikuwa na  majeraha ya risasi huku wakiwa hawawezi kusimama na kuongea vizuri ambapo katika kuwahoji zaidi, walisema wamepigwa risasi na polisi katika pori la Mwanduhubandu lililopo Kijiji cha Mpeta, Uvinza

Katika kesi hiyo, Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi ambayo anadaiwa kuyatenda tarehe 28 Oktoba 2018  katika mkutano na waandishi wa habari, uliyofanyika kwenye Makao Mkuu ya Ofisi ya Chama cha ACT Wazalendo.