Si kila aliyehusika katika ajali hii alikwenda kuchota mafuta - Rais Magufuli


Rais John Pombe Magufuli amewataka raia nchini kutowahukumu waathirika wa mkasa wa moto uliosababisha vifo vya watu 69 mjini Morogoro siku ya jana. Amesema kwamba huu sio muda wa kulaumiana na badala yake akawashukuru baadhi ya Watanzania waliojitolea kuokoa maisha ya watu.

Akizungumza baada ya kuwasili katika hospitali ya Taifa Muhimbili ili kuwajulia hali majeruhi, Magufuli amesema kuwa baadhi ya walioathirika na mkasa huo walikuwa wamekwenda eneo la tukio ili kutoa msaada huku wengine wakiwa wapita njia.

''Ninasisitiza, tusiwe majaji, tusiwe wepesi kutoa hukumu, si kila aliyehusika katika ajali hii alikwenda kuchota mafuta, wengine walikuwa wanapita tu, wengine walikwenda kuokoa, wengine walikuwa na shughuli zao. Mwingine alikuwa safarini kuelekea Mtwara, akazuiliwa na moto ulipolipuka ukamkuta'', alisema Rais Magufuli..

Hatua hiyo inajiri baada ya Jukwaa la Wahariri nchini kusema kwamba vifo hivyo vimetokana na tabia mbaya miongoni mwa watu wanaochukulia ajali kama fursa ya kujipatia mali kwa njia haramu ilioanza katika miaka ya hivi karibuni.