TAKUKURU yaokoa bilioni 86 tangu mwaka 2015


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa nchini (Takukuru) imeokoa kiasi cha shilingi bilioni 86 zilizotokana na ukwepaji kodi na makosa mbalimbali ya ufisadi tangu mwaka 2015.

Hayo yameelezwa Jumamosi hii na msemaji wa msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika mjini Dodoma.

Dk Abbas amesema kati ya fedha hizo,  Shilingi bilioni 14.6 zimerudishwa serikalini kwa kuwa zimepatikana katika uhalifu na shilingi bilioni 10 zimerudishwa tena serikalini baada ya kuuza magari, nyumba na vituo vya mafuta.

“Takukuru pia wamerejesha zaidi ya Shilingi bilioni 25 zikiwemo fedha zilizopatikana kwa rushwa baada ya washtakiwa kukutwa na hatia, fedha hizo zinarudi kwa Watanzania,” amesema Dk Abbas.

Pia ameongeza kuwa Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA)  imeokoa kiasi cha shilingi bilioni 46.8 zilizotokana na mikataba mibovu waliyoibaini wakati wa ukaguzi.