Wanaosambaza picha za marehemu katika mitandao kuchukuliwa hatua


Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amelitaka Jeshi la Polisi nchini kuwakamata na kuwachukulia sheria wale wote wanaosambaza picha za marehemu katika mitandao ya kijamii kwani kufanya hivyo nikosa kisheria

Masauni ametoa kauli hiyo Mjini Morogoro ambapo amesema kuwa kusambaza picha za marehemu katika mitandao ya kijamii ni kuwadhalilisha wahusika na ni uvunjaji wa sheria za nchi.

“Ninaziagiza mamlaka na vyombo vinavyohusika vihakikishe vinafuatilia na kuchukua hatua kwa wale ambao wanakiuka sheria za nchi yetu kwa kusambaza mitandaoni picha za marehemu,” aliagiza Masauni.

Aidha Masauni amesema siyo vema kuanza kutumia majanga ya Kitaifa kama ajali ya moto iliyotokea Mkoani Morogoro na kusababisha watu zaidi ya 70 kufariki dunia ndani ya muda mfupi hivyo kuanza kusambaza picha za waathirika mitandaoni kwa dhamira ya kudhalilisha sio jambo la busara.

“Watu hawa wamefariki dunia na mtu yeyote katika tukio lile angekufa, mimi au wewe, ndugu yako au jamaa yako, fikiria kama ni jambo limekukuta au ndugu yako halafu ukachukua picha na kuisambaza kwenye mitandao, katika mazingira kama yale,” Masauni alisema.