Na Thabit Madai,Zanzibar
Mkutano wa Kumi na Tano Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar unatarajiwa kuanza siku ya Juma tano Septemba 18 kuanzia majira ya Saa tatu kamili za Asubuhi.
Akitoa Taarifa kwa vyombo vya habari, Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Raya Issa Mselem alisema kuwa Mkutano huo unatarajiwa kuanza kwa shughuli mbali mbali ikiwemo maswali na majibu na kusomwa kwa mara ya Pili Miswada ya Sheria.
Alisema Jumla ya Maswali 137 yanatarajiwa kuulizwa na wajumbe wa baraza la wawakilishi na kupatiwa majibu kutoka kwa Mawaziri wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Mbali na Maswali na majibu katika mkutano huo shughuli nyingine itakuwa kusomwa kwa mara ya Pili Miswada ya Sheria mbali mbali ya Sheria ikiwemo Mswada wa Kufutwa sheria ya viongozi wa kitaifa na kutunga sheria ya kuanzisha jumuiya ya mawakili Zanzibar ambao utaweka utekelezaji wa Malengo na Shughuli za jumuia hiyo”alisema Katibu huyo.
Alisema kuwa mswada mwingine ni mswada wa Sheria ya utawala wa baraza la wawakilishi na mambo mengine yanayohusiana na hayo.
“Aidha Mswada mwingine ni mswada wa Sheria ya kuanzisha jumuiya ya mawakili Zanzibar, kuweka malengo ya utekelezaji wa shughuli za jumuiyana mambo mengine yanayoyohusiana na hayo” alisema katibu Raya.
Aliongeza kwa kusema kuwa katika Mkutano huo kutawasilisha ripoti za Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu utekelezaji wa maagizo ya Kamati za kudumu za Baraza la Wawakilishi kwa mwaka 2018/19.