Na Ahmad Mmow, Lindi.
Jumuia ya Jamiiyatul Akhalaaqul Islam ya mkoa wa Lindi imefanikiwa kukusanya uniti 767 za damu salama kwa kipindi cha miaka minne.
Hayo yameelezwa na katibu wa jumia hiyo, Said Makambo, leo mjini Lindi. Alipozungumza na Muungwana Blog baada ya kumalizika zoezi la uchangiaji damu kupitia maadhimisho ya kumbukumbu ya kuuwawa kwa mjukuu wa Mtume Muhammad S.A.W, imam Hussain.
Alisema tangu mwaka 2015 hadi leo imefanikiwa kukusanya lita 767 za damu salama, ambazo zimepelekwa katika vituo mbalimbali ya kutolea huduma za afya ili iwasaidie wenye uhitaji.
Alisema jumuia hiyo inatambua kwamba kunauhitaji mkubwa wa damu kwa wagonjwa. Ambapo imani yao ya dini ya kiislam inawataka kuwahurumia na kuwasaidia wagonjwa. '' Dawa na vifaa tiba vinaweza kununuliwa, lakini damu haiuzwi na haitengenezwi. Lakini sisi wanadamu tunayo na hatukununua, bali tumepewa bure, kwahiyo tunatakiwa kutoa bure,'' alisema Makambo.
Aliweka wazi kwamba niukatili mkubwa kusiki wagonjwa wanafariki kwasababu ya kukosa damu ambayo kila mtu anayo na hakununua.
'' Mbali na kuchangisha na kukusanya damu, pia tunazika watu wasio na ndugu kwa kugharamia mazishi yao. Tangu mwaka 2014 hadi leo tumezika watu 14, kwahiyo jamii inatakiwa kuwa na huruma kwa kusaidia kila mwenye uhitaji bila kujali dini, kabila wala rangi,'' alisisitiza Makambo.
Katika hafla ya uchangiaji wa leo iliyofanyika katika viwanja vya msikiti wa dhehebu la Khoja Shia Ithiaanasheri Jamaat, zimekusanywa uniti kumi za damu salama.
