Na Thabit Madai, Zanzibar
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib Unguja, Ayoub Muhamed Mahmoud ameliagia Jeshi la Polisi ndani ya Mkoa huo kumueka ndani Ali Halfani Salum maarufu Ali mchawi kwa kujihusisha na uuzaji wa viwanja katika heka na shamba kwenye maeneo mbali mbali ya Wilaya ya Magharibi “A” na kusababisha migogoro ya ardhi.
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi ambae pia ni Mwenyekiti wa kamati ya usalama ya Mkoa huo Ayoub Mohammed Mahmoud ametoa agizo hilo katika ziara maalum iliyoshirikisha kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa huo kutatua migogoro ya ardhi katika Shehia Mbuzini na Mwakaje kufuatia malalamiko yaliopo kutoka kwa wananchi wa maeneo hayo.
Amesema agizo la kumuweka ndani Nd Ali Halfan Saluum maarufu Ali Mchawi ni kutokana na mamlaka ya kisheria aliyonayo kwa mujibu wa sheria ya Tawala za Mikoa na serikali za mitaa akiwa Mkuu wa Mkoa na sheria ya baraza la usalama la taifa akiwa mwenyekiti wa kamati ya ulizi ya Mkoa huo kwa kuona uvunjifu wa amani anaoufanya muhisika huyo kwa kuuza viwanja kinyume na utarabu.
“Nikiwa Mkuu wa Mkoa huu ni kiongozi wa wananchi na Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa ninayo mamala ya kisheria ya Tawala za Mikoa kama Mkuu wa Mkoa lakini pia nikiwa Mwenyekiti wa usalama naliagiza jeshi la polisi limuweke ndani Ali mchawi maana amekuwa akitajwa katika kesi nyingi za uuzaji wa viwanja kinyume na utaratibu na kusababisha migogoro mingi katika Mkoa wetu,” alisema Ayoub.
Aidha Mkuu wa Mkoa amazuwia ujenzi wa nyumba za makaazi na shughuli nyengine isipokuwa kilimo katika eka ya Bi Rabia Seif iliyopo Shehia ya Mwakaje na ekka ya Tatu iliyopo Shehia ya Mbuzini ambazo kwa kiasi kikubwa zimevamiwa kwa ujenzi wa nyumba za makaazi jambo ambalo linaenda kinyume na malengo ya matumizi ya ardhi.
Hata hivyo Ayoub amewaagiza viongozi wa shehia hizo kufanya tathmini ya nyumba na misingi iliyojengwa katika ekka hizo na kufuta agizo lililotolewa la kukatwa eka ya tatu na nusu yake kupewa Ali mchawi na badala yake ibaki kwa mmiliki wa awali kwa madhumuni yaliyokusudiwa.
Katika hatua nyengine Mkuu wa Mkoa ameuagiza uongozi wa serikali ya Wilaya ya Magharibi “A”kukaa pamoja na wananchi wa kijiji cha Kitundu Shehia ya Mwakaje na msimamizi wa ekka ya Thelesia Albano Ally kutatua malalamiko yaliopo ya kujengwa kwa barabara iliyopita katikati ya eka hiyo bila ya makubaliano na mmiliki wa heka hiyo.
“Naomba Mkuu wa Wilaya kakae nao pande zote mbili hizi kwa maana mlalamikaji na waliolalamikiwa tulipatie ufumbuzi tatizo hili tunajua maendeleo tunayataka lakini pia na migogoro isiwepo ili tutengeneze ule ustawi wa jamii hapa tusilete maandeleo lakini pia tukatengeneza chuki kwa wananchi wetu,”alisema Ayoub.
Mapema akizungumza katika ziara hiyo afisa kutoka Idara ya mipango miji na vijiji kamisheni ya ardhi Mohammed Badrudiddin amesema kuwa mwaka 2015 kulitayarishwa mpango mkuu wa matumizi ya ardhi na endapo mtu yeyote anaetaka kubadilisha matumizi ya ardhi lazima aombe idara husika kwa ajili ya kupima na kupangwa kwa matumizi yaliyokusudiwa.
Nae msimamizi wa ekka ya Theresia Albano Ally Ndugu Mahmoud Peter amesema kitendo cha kupitishwa ujenzi wa barabara katika eneo la ekaa yao hakukuwa na taarifa yeyote wala makubaliano yaliyofikiwa na imejengwa bila ya ridhaa ya mmilikiwa wa ekaa hiyo.
“Nimeleta malalamiko ya kupitishwa njia katikati ya shamba letu bila ya kupewa taarifa na kukubaliana,nilisikia kuwa kunataka kupitishwa baarabara na nikawafata wahusika na kuwaeleza na kuonesha ambapo sisi tunataka ipitishwe njia hiyo lakini bado wameamua kupitisha hapa ambapo hatukupataka” alisema Mahmoud.
