Wafanyabishara jijini Dodoma wameaswa kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na taasisi za kifedha ili waweze kunufaika na ongezeko kubwa la fursa za kibiashara zinazoibuka katika jiji hilo ambalo ni makao makuu ya nchi.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Bilinith Mahenge katika hotuba iliyosomwa na Mkurugenzi wa Jiji hilo, Godwin Kunambi.
“Dodoma kwa sasa kuna utekelezaji wa miradi mikubwa mingi ikiwemo barabara, stendi ya mabasi ambayo ni kubwa zaidi Afrika Mashariki, upanuzi wa uwanja wa ndege, ujenzi wa viwanja vya mapumziko ambayo vitachochea mzunguko mkubwa wa pesa na ongezeko la watu," amesema.
"Hivyo ni fursa kwa wafanyabiashara kushirikiana vyema na benki kama NBC ili kukuza mitaji itayowawezesha kufanya uwekezaji utakaowanufaisha na mabadiliko hayo,’’ alisema.
Akizungumza kuhusu uanzishwaji wa klabu hiyo, Mkuu wa Kitengo cha wateja wa kati na wadogo wa benki ya NBC, Evance Luhimbo alisema pamoja na mambo mengine klabu hizo zinalenga kutoa mafunzo kwa wateja wa benki hiyo kuelewa mabadiliko ya uboreshwaji wa huduma za za benki hiyo, kuwakutanisha pamoja wajadili fursa za kibiashara sambamba na kuwajengea uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya kibiashara ikiwemo masuala ya kodi na taratibu za kijiunga na taasisi wadau biashara ili ziwasaidie.
