FIFA yashusha rungu baada ya mashabiki kuzomea ulipopigwa wimbo wa taifa



Shirikisho la Soka la Hong Kong jana lilipigwa faini na FIFA baada ya mashabiki kubeza na kuzomea ulipopigwa wimbo wa taifa wa China wakati inaanza mechi ya michuano ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Iran.

Kamati ya Nidhamu ya FIFA imelitoza shirikisho hilo faini ya euro 13,700 na kuwaonya mashabiki kwa kufanya fujo wakati wimbo wa taifa unaimbwa na kutumia vitu kutuma ujumbe ambao haufai kwenye matukio ya michezo.

 Hong Kong imeingia kama timu inayojitegemea lakini kwa vile ni Mkoa wa Utawala maalumu wa China, wimbo wa taifa wa China huwa unapigwa kabla ya mechi. Hong Kong ipo nafasi ya tatu kwenye Kundi C la michauno ya Asia na baada ya mechi hiyo ya jana, mechi itakayofuata ya nyumbani itakuwa dhidi ya Bahrain Novemba 14 mwaka huu.