Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dk. Rhimo Nyansaho (Mb), tarehe 12 Machi,2026, katika ofisi ndogo za Wizara ya Ulinzi na JKT, Upanga, jijini Dar es Salaam amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Kikosi cha Ulinzi cha Jimbo la Nebraska nchini Marekani (Nebraska National Guard), Meja Jenerali Craig Strong, aliyeambatana na Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini, Mhe. Andrew Lentz, pamoja na maafisa jenerali kadhaa kutoka Nebraska.
Baada ya mazungumzo hayo, Waziri wa Ulinzi na JKT pamoja na Kaimu Balozi Lentz walishuhudia utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya JWTZ na Jeshi la Marekani uliotiwa saini na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda pamoja na Meja Jenerali Strong. Mkataba huo, pamoja na mambo mengine, unalenga kudumisha mahusiano ya muda mrefu kati ya majeshi yetu na nchi zetu kwa ujumla ambayo awali yaliasisiwa mwanzoni mwa miaka ya 1960 na viongozi wetu hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati John Fitzgerald Kennedy.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano ya ushirikiano kati ya JWTZ na Jeshi la Marekani, Waziri wa Ulinzi na JKT, Mhe Rhimo Nyansaho amelipongeza Jeshi la Ulinzi wa Tanzania na Jeshi la Ulinzi la Marekani la Nebraska kwa kufikia hatua hiyo muhimu ya kihistoria katika sekta ya Diplomasia ya Ulinzi na akamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungno wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake yaliyohakikisha makubaliano hayo yanasainiwa na kuanza kutekelezwa.
Baadhi ya manufaa yatakayotokana na makubaliano haya ni pamoja na kufanya mazoezi ya pamoja, mafunzo, kubadilishana uzoefu pamoja na kushirikiana katika huduma za matibabu.
Waziri wa Ulinzi na JKT akaongeza kwa kusema imeridhishwa na hatua hiyo ambayo inayoakisi na sera ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Rais Samia Suluhu Hassan katika kudumisha mahusiano ya kimataifa na akaahidi kuhakikisha makubaliano haya yanatekelezwa kwa faida ya nchi za Tanzania na Marekani na watu wake.



0 Maoni