Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda, amejiunga rasmi katika kinyang’anyiro cha kuwania ubunge wa Jimbo la Isimani kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, William Vangimembe Lukuvi, kilichotokea Machi 25, 2026.
Jumla ya wagombea 18 wamejitokeza kuchukua na kurejesha fomu za kuwania nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika zoezi lililofanyika kwa siku mbili kuanzia Aprili 17 hadi 18, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 18, 2026, Katibu wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wilayani humo, Sure Mwasanguti, alisema kati ya wagombea hao, wanawake ni wawili huku wanaume wakiwa 16.
Amesema zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu limekamilika na sasa linapisha hatua nyingine za mchakato wa kumpata mgombea atakayewakilisha chama hicho katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.
Miongoni mwa waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ni Fred Fabian Ngajiro (Vunjabei), Festo Shemu Kiswaga, Asakwe Lameck Widambe, Arif Ally Abri, Eng. Sebastian Antony Kiyoyo, Tumaini Godwin Msowoya na Watende Gwerino Kiyagi.
Wengine ni Lazaro Francis Ngwira, David Evance Komba, Thobias Karlo Mwilapwa, Titho Maulilyo Cholobi, Emmanuela Kaganda Mtatifikolo, Claudio Francis Nzwaga, Josephat Gwelino Msambwa, Elias Lupituko Migodela Kazikuboma, Egidy Stanslaus Mkolwe, Dk. Abdallah Suleiman Lusasi na Tedson Johansery Ngwale.
Jimbo la Isimani sasa linasubiri hatua zinazofuata za uteuzi wa mgombea wa CCM kabla ya kuelekea kwenye uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi iliyoachwa wazi.
0 Maoni