Jamii, serikali na wadau wa elimu wanavyoshirikiana kukabiliana na ongezeko la wanafunzi litakalotokana na wanafunzi wa darasa la sita na la saba kuingia kidato cha kwanza kwa pamoja mwaka 2028
Na John Walter – Manyara
![]() |
| "Wananchi wa Kata ya Magugu wakishiriki ujenzi wa madarasa ili kujiandaa na ongezeko la wanafunzi litakalotokana na utekelezaji wa sera mpya ya elimu." |
Tanzania ipo katika kipindi muhimu cha mageuzi ya elimu yanayolenga kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kujifunza kwa muda mrefu zaidi na kupata maarifa yanayomwandaa kukabiliana na mahitaji ya dunia ya sasa.
Kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la
2023, serikali imefanya maboresho makubwa ya mfumo wa elimu kwa kuongeza elimu
ya lazima kutoka miaka saba hadi miaka 10. Maboresho hayo yanalenga kuhakikisha
watoto wengi zaidi wanapata elimu ya sekondari, kuimarisha usawa katika elimu
na kuwajengea wanafunzi maarifa, ujuzi na stadi za maisha zitakazowawezesha
kujitegemea.
Tofauti na mfumo wa zamani ambao ulitambua darasa la saba
kama mwisho wa elimu ya lazima, mfumo mpya unapanua wigo huo hadi ngazi ya
sekondari. Aidha, maboresho hayo yanaweka mkazo katika elimu ya ujuzi, ubunifu,
ujasiriamali na matumizi ya maarifa katika kutatua changamoto za maisha badala
ya kutegemea elimu ya taaluma pekee.
Hata hivyo, pamoja na matarajio makubwa ya sera hiyo,
utekelezaji wake umeibua changamoto mpya inayohitaji maandalizi ya haraka ya
miundombinu ya elimu.
Mwaka 2028, Tanzania itashuhudia hali ya kipekee ambapo
wanafunzi wa darasa la sita wanaohitimu kupitia mfumo mpya na wanafunzi wa
darasa la saba wanaomaliza mfumo wa zamani wataingia kidato cha kwanza kwa
wakati mmoja. Hali hiyo inayojulikana kama “double cohort” inatarajiwa kuongeza
kwa kiasi kikubwa idadi ya wanafunzi watakaojiunga na shule za sekondari
nchini.
Ongezeko hilo lina maana moja kubwa; hitaji la madarasa
zaidi, walimu zaidi, vitabu zaidi na mazingira bora zaidi ya kujifunzia.
Bila maandalizi ya kutosha, shule nyingi zinaweza
kukabiliwa na mrundikano wa wanafunzi madarasani, hali inayoweza kuathiri ubora
wa elimu na ufanisi wa ufundishaji.
Katika maeneo mbalimbali nchini, maandalizi tayari
yameanza. Miongoni mwa maeneo yanayoonesha mfano wa namna jamii inavyoweza
kushiriki katika utekelezaji wa sera mpya ni Kata ya Magugu, Wilaya ya Babati
mkoani Manyara.
Katika kata hiyo, mjadala wa elimu umehamia kwenye jambo
moja kubwa; madarasa.
Si kwa sababu shule zimefungwa. Si kwa sababu wanafunzi
wamepungua. Bali kwa sababu mwaka 2028 unakuja na changamoto ambayo haijawahi
kushuhudiwa katika historia ya hivi karibuni ya elimu nchini.
Kwa mwanafunzi wa shule ya msingi, Shamila Juma,
utekelezaji wa sera mpya una maana moja kuu; watoto wengi zaidi watapata nafasi
ya kuendelea na elimu ya sekondari.
"Elimu ya sekondari ni muhimu kwa sababu inamfanya
mtu aweze kujitambua na kujitegemea," anasema.
Mawazo hayo yanaungwa mkono na mwenzake John Bayyo ambaye
anaamini elimu ya sekondari ndiyo daraja la kuwapa vijana stadi za maisha na
kuwaandaa kwa maisha ya baadaye.
Lakini wakati wanafunzi wakiona fursa, viongozi wa elimu
wanaona changamoto kubwa inayohitaji maandalizi ya haraka.
Katika Shule ya Sekondari Magugu Day yenye wanafunzi zaidi ya 1,000, tayari dalili za changamoto hiyo zinaonekana.
Mkuu wa shule hiyo, Revokati Kimario, anasema shule hiyo
kwa sasa ina upungufu wa madarasa saba.
Anabainisha kuwa mwaka 2026 shule ilipokea wanafunzi 338
wa kidato cha kwanza. Hata hivyo, makadirio yanaonesha kuwa mwaka 2028 shule
hiyo inaweza kupokea wanafunzi zaidi ya 600.
Hii ni ongezeko la zaidi ya asilimia 77 ndani ya kipindi
cha miaka miwili.
Kwa lugha rahisi, kama maandalizi hayatafanyika mapema,
wanafunzi wengi zaidi wataingia katika madarasa yale yale yaliyopo sasa.
Matokeo yake yanaweza kuwa mrundikano wa wanafunzi,
kupungua kwa ufanisi wa ufundishaji, changamoto za usimamizi wa masomo na
mazingira magumu ya kujifunzia.
Tatizo hilo si la Magugu pekee.
Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Mji wa Babati,
Paskalina Lowekelo, anasema halmashauri hiyo ina upungufu wa madarasa 60.
Kwa mujibu wake, changamoto hiyo imekuwa sehemu ya
mjadala katika vikao vya wadau wa elimu vinavyoangalia namna ya kujiandaa na
ongezeko la wanafunzi linalotarajiwa.
"Baadhi ya madarasa yatakayobaki wazi katika shule
za msingi yanaweza kutumika kwa muda. Pia tumekuwa tukijadili namna ya kutumia
uwezo uliopo katika baadhi ya shule za sekondari binafsi zenye wanafunzi
wachache ili kupunguza shinikizo la wanafunzi watakaoingia kidato cha
kwanza," anasema.
Kauli hiyo inaonesha kuwa changamoto ya mwaka 2028
haiwezi kutatuliwa na taasisi moja pekee, bali inahitaji ushirikiano wa
serikali, sekta binafsi na jamii.
Lakini kinachoifanya Magugu kuwa mfano wa kipekee si
ukubwa wa changamoto, bali namna wananchi walivyoamua kuikabili.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Magugu, Mary Simba, anasema
kata hiyo inatarajiwa kuwa na upungufu wa vyumba 25 vya madarasa ifikapo mwaka
2028.
Kata hiyo inayojumuisha shule za sekondari za Magugu,
Matufa, Gichameda na Sarame ndiyo kata kubwa zaidi katika Wilaya ya Babati.
Badala ya kusubiri kila kitu kifanywe na serikali,
wananchi waliamua kuchukua hatua.
Kupitia mikutano ya vijiji iliyoandaliwa na Kamati ya
Maendeleo ya Kata, wakazi walikubaliana kuchangia shilingi 10,000 kwa kila kaya
ili kusaidia ujenzi wa madarasa.
Uamuzi huo unaweza kuonekana mdogo kwa mtu wa nje, lakini
ndani yake umebeba ujumbe mkubwa; jamii imeanza kuiona sera ya elimu kama
jukumu lake pia.
Diwani wa Kata ya Magugu na Mwenyekiti wa Kamati ya
Maendeleo ya Kata, Stanley Charles, anasema michango hiyo ilianza Mei 15 na
itaendelea hadi Julai 2026 huku ujenzi ukitarajiwa kuanza mwezi Agosti.
Anasema viongozi wa kata wameamua kuanza maandalizi
mapema ili ifikapo mwaka 2028 changamoto ya madarasa isiwe kubwa kama
inavyohofiwa sasa.
Kwa zaidi ya kaya 5,102 zilizopo Magugu, mchango huo
unaweza kuzalisha nguvu kubwa ya kifedha kwa ajili ya maandalizi ya mwaka 2028.
Kwa sasa baadhi ya wazazi tayari wanashiriki katika
ujenzi hadi kufikia hatua ya upauzi wa majengo ambapo boma moja linagharimu
takribani shilingi milioni 12.5.
Kasimu Bakari ni miongoni mwa wananchi waliounga mkono
mpango huo.
Kwake, elimu si jukumu la serikali pekee.
"Hakuna ombi hapa. Lazima tujenge kwa ajili ya
watoto wetu. Watoto ni wetu," anasema.
Naye Mwanahamisi Hussein anaunga mkono jitihada hizo
lakini anashauri kuwe na uratibu mzuri wa michango ya maendeleo.
"Tuko tayari kuchanga, lakini michango mingine
ipunguzwe ili wananchi wabaki na nguvu ya kushiriki katika ujenzi wa
madarasa," anasema.
Maoni hayo yanaonesha kuwa wananchi wako tayari kushiriki
katika utekelezaji wa sera mpya mradi washirikishwe na waone matokeo ya
michango yao.
Katika ngazi ya taifa, serikali imeendelea kusisitiza
kuwa utekelezaji wa sera hiyo unaenda sambamba na maandalizi ya miundombinu na
rasilimali watu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema mwaka 2027/2028 wanafunzi wa darasa la sita na darasa la saba wataingia sekondari kwa pamoja kutokana na mabadiliko ya mfumo wa elimu.
Amesisitiza kuwa maandalizi ya mapema ni muhimu ili
kukabiliana na changamoto za madarasa, walimu na miundombinu mingine
inayohitajika katika utekelezaji wa sera hiyo.
Katika kuimarisha utekelezaji wa mtaala mpya, serikali
pia inatarajia kuajiri walimu 4,000 wa masomo ya biashara ili kuwajengea
wanafunzi maarifa ya ujasiriamali na kuwawezesha kujitegemea baada ya masomo
yao.
Hatua hiyo inaendana na lengo kuu la maboresho ya elimu;
kuhamisha msisitizo kutoka elimu ya taaluma pekee kwenda elimu inayojenga
ujuzi, ubunifu na uwezo wa kujiajiri.
Katika Shule ya Sekondari Kiru, maandalizi ya utekelezaji wa sera mpya tayari yanaonekana.
Mkuu wa shule hiyo, Isaack Makena, anasema serikali
imejenga madarasa matano ya ziada, imetoa vitabu 1,100 vya mtaala mpya
ulioboreshwa na kuongeza walimu watano.
Kwa mtazamo wake, mtaala mpya utawasaidia wanafunzi
kujifunza kwa vitendo zaidi na kuwawezesha kujiandaa vyema kwa maisha ya
baadae.
Mtazamo huo unaungwa mkono na mchambuzi wa masuala ya
elimu, Lucas Alphonce, ambaye anaamini Tanzania imefika wakati wa kufanya
mageuzi hayo ili kuendana na nchi nyingine zilizotangulia katika mfumo huo.
Anasema maboresho hayo yanaweza kusaidia kuandaa vijana
wenye uwezo mkubwa wa kujitegemea na kushiriki katika maendeleo ya uchumi wa
taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Sayansi za
Afya Haydom, Bathomolayo Madangi, anasema mtaala mpya unapaswa kuendelea
kuzingatia stadi za maisha, ujasiriamali na uwezo wa wanafunzi kujiajiri.
Anaamini mafanikio ya sera mpya hayatapimwa kwa idadi ya
wanafunzi wanaohitimu pekee, bali kwa uwezo wao wa kutumia maarifa
waliyojifunza kutatua changamoto za maisha.
Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2023 imekusudia
kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya elimu kwa usawa na kwa muda mrefu
zaidi.
Lakini sera yoyote, hata ikiwa nzuri kiasi gani, haiwezi
kufanikiwa bila ushiriki wa jamii.
Mfano wa Magugu unaonesha kuwa mafanikio ya sera hayawezi
kutegemea serikali pekee. Yanahitaji ushiriki wa wazazi, viongozi wa jamii,
sekta binafsi na wadau wa maendeleo.
Wakati wengine wakisubiri kuona nini kitatokea mwaka
2028, wananchi wa Magugu tayari wanachanga fedha, wanajenga madarasa na
wanashiriki katika kupanga mustakabali wa watoto wao.
Pengine mafanikio makubwa ya sera hii hayatakuwa idadi ya
madarasa yatakayojengwa au walimu watakaoajiriwa.
Mafanikio yake yatakuwa pale ambapo wananchi wataacha
kuiona elimu kama jukumu la serikali pekee na kuanza kuiona kama uwekezaji wao
wenyewe.
Katika Kata ya Magugu, safari hiyo tayari imeanza kwa
shilingi elfu kumi tu kutoka kila kaya, lakini thamani yake inaweza kuwa kubwa
zaidi kuliko fedha hizo; ni uwekezaji katika kizazi kijacho cha Tanzania.



.jpeg)
0 Maoni