Hospitali kuwajengea vyoo shule ya msingi Mloganzila

Hospitali ya Taifa Muhimbili –Mloganzila imedhamiria kujenga vyoo matundu matano katika Shule ya Msingi Mloganzila ikiwa ni kuunga mkono juhudi zinazofanywa na uongozi wa shule hiyo ya kuboresha mazingira ya shule ili wanafunzi wasome katika sehemu safi na salama.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es salaam na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi alipokua akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Lawrence Museru katika mahafali ya 14 ya darasa la saba ya Shule ya Msingi Mloganzila.


Dkt. Magandi ameeleza kuwa ujenzi wa vyoo utagharimu shilingi milioni 10 na
kwamba utaanza mara moja ambapo vyoo vinne vitakua vya wasichana na kimoja ni kwa ajili ya watoto wenye ulemavu.

“Tulielezwa kuna hitajika matundu kumi ya vyoo hivyo kama taasisi tukaona ni vema kusapoti suala hili ili kuhakikisha watoto wetu wanasoma katika mazingira safi, pia tumefanikiwa kutafuta mfadhili ambaye amekubali kujenga matundu mengine matano kwa maana hiyo matundu kumi yaliyohitajika yatakua yamekamilika” amefafanua Dkt. Magandi.


Dkt. Magandi ametumia fursa hiyo kuikumbusha jamii kwamba jukumu la maendeleo ya elimu ni la wananchi wote hivyo kila mmoja anapaswa kushiriki kikamilifu.

Pia ametoa wito kwa wazazi katika kipindi hiki ambacho wanafunzi wanasubiri matokeo ya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi waendelee kuwalea na kuwalinda watoto ili wasijihusishe katika vitendo viovu ambavyo vitaharibu maisha yao.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mloganzila Mwalimu Geofrey Magembe ameishukuru Muhimbili-Mloganzila kwa msaada wa ujenzi wa vyoo na kueleza kuwa shule hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa vyoo na uchakavu wa majengo.

Katika mahafali hayo takribani wanafunzi 100 wametunukiwa vyeti vya kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2019.