Kanisa katoliki parokia ya Makanya limelishukuru shirika la Kuhamasisha Jamii Itambue Haki na Sheria( CHPO) la wilayani Nanyumbu kwa kusuluhisha mgogoro wa ardhi baina ya kanisa hilo na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Makanya, wilaya ya Nanyumbu mkoa wa Mtwara.
Shukrani hizo zilitolewa jana kijijini Makanya na padre Jacob Mchopa, alipozungumza na Muungwana Blog.
Padre Mchopa alisema mgogoro baina ya kanisa na baadhi ya wananchi waliojenga nyumba za makazi katika eneo la kanisa ulikuwa mkubwa. Kwani ulifikia hatua ya kufikishwa mahakamani na baadhi ya wananchi hao.
Alisema pamoja na mgogoro huo kuwa mkubwa, wasaidizi wa kisheria wa CHPO wameweza kusuluhisha na kumaliza kwa amani.
'' Ninawashukuru sana, eneo lililochukuliwa ni mali ya kanisa lina hati ya kumiliki kwa muda wa miaka 99, toka mwaka 1959. Lakini baadhi ya watu wamejenga, tulipowaambia waondoke walikataa katakata wakidai waliuziwa na mmoja wa watumishi wa parokia ya Makanya. Lakini wasaidizi walitukutanisha, nashukuru sana. Kwani tayari tumeelewana,'' alisema Paroko Mchopa.
Aliyataja makubaliano yaliyoafikiwa na pande zote ni kanisa kuwarejeshea fedha zao. Kila mmoja kiasi cha fedha alizonunulia.
Huku akitoa wito kwamba kila anayehitaji kuongezewa muda wakuishi katika eneo ambalo ametakiwa kuhama atume barua ya kuomba kuongezewa muda na apeleke kwa kanisa hilo. '' Sisi kanisa tunahubiri upendo na amani, ndio maana tumekubali kuwarejeshea fedha zao ingawa waliuziwa na mtu nasio kanisa.
Kwasasa tumekubaliana hadi mwakani, tarehe 20, Januari waachie maeneo hayo. Kama kuna anayetaka kuongezwa muda alete barua kwetu na aoneshe anaomba kuendelea kuishi kwa muda gani,'' alisema Mchopa.
Kuhusu mahusiano na jamii baada yakusuluhishwa alisema mahusiano ni mazuri sana wananchi wanashirikiana naye binafsi na kanisa. Akiweka wazi kwamba hata walioanza kuacha maeneo hawaoneshi kinyongo wala chuki.
Mmoja wa wanaotakiwa kuachia eneo alilojenga, Omari Hausi alisema wamepokea uamuzi uliotolewa tarehe 20.9.2019 katani Nangomba ambao ulilenga kusuluhisha mgogoro huo. Huku akisema maeneo hayo waliuziwa na kamati ya walei ya parokia ya Makanya.
'' Kwenye kikao kile tulibaini eneo hili ni mali ya jimbo nasiyo kamati iliyotuuzia. Hata hivyo kanisa limekubali kuturejeshea fedha zetu nalinafikiria kutuongezea muda wa kuishi, ni jambo jema tunashukuru,'' alisema Hausi.
10: Nae mkurugenzi wa CHPO, Michael Mkumba alisema wananchi wilayani Nanyumbu wameanza kujua umuhimu wa kituo hicho. Watu wengi wameanza kwenda kuomba ushauri kwenye kituo hicho badala ya kukimbilia mahakamani.
Maelezo ambayo yaliungwa mkono nakatibu tawala wa wilaya (DAS) hiyo, Salum Palango ambae ofisi yake ipo bega kwa bega na shirika hilo.
Akiweka wazi kwamba limesaidia kusuluhisha na kupunguza migogoro katika wilaya hiyo ya Nanyumbu.
