https://monetag.com/?ref_id=TTIb Taasisi ya Jasiri Asili yatoa elimu ya kufikia ndoto Msalato Sekondari | Muungwana BLOG

Taasisi ya Jasiri Asili yatoa elimu ya kufikia ndoto Msalato Sekondari



Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.

Katika kuunga mkono juhudi za Serikali kutoa elimu bure na kuhakikisha mtoto wa kike anafikia malengo, Taasisi ya Jasiri Asili imefanya ziara katika shule kongwe ya Msalato jijini Dodoma na kutoa elimu ya afya, kujitambua na kuwapa mbinu mbalimbali wanafunzi wa Shule hiyo katika kufikia malengo yao.

Akizungumza na wanafunzi shuleni hapo ikiwa ni mwendelezo wa siku ya mtoto wa kike, mwanzilishi wa taasisi hiyo, Marietha Lugola amesema wameamua kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi wa jinsia zote ili kuwasaidia kutimiza ndoto zao na kunufaika na mpango wa elimu bila malipo.


" Niwasihi msikubali kuharibiwa ndoto zenu, Rais Magufuli ametoa fursa ya kila mtoto kusoma kupitia sera yake ya Elimu bure hivyo msimuangushe. jivunieni usichana wenu, jipeni thamani ili muweze kutimiza ndoto zenu na kuisaidia nchi yetu," Amesema Marietha.

Amebainisha kuwa lengo lao ni kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwainua vijana wa kiume na kike kielimu, kuwakomboa kifikra na kuwawezesha kufikia malengo yao ili waje kuwa msaada kwenye familia zao na taifa.

Amewataka wanafunzi hao kutumia elimu yao kusaidia jamii zinazowazunguka katika kupiga vita mila potofu kwa watoto wa kike kama ukeketaji, ndoa za utotoni ambazo zimekua zikichangia kurudisha nyuma maendeleo ya elimu kwa watoto wa kike.

"Serikali yetu imetoa mwanga mkubwa kwenye suala la elimu, hii sera ya elimu bure imekua msaada kwa watoto wengi sana hasa wanaotoka katika familia zisizojiweza,  na jukumu letu na sisi pia tuoneshe mchango wetu kwa kuwaongezea maarifa na kuwasaidia kuziona fursa ambazo zinaweza kuwa msaada kwenye maisha yenu" amesema.

Pia amewasihi kuachana na makundi yasiyo na msingi mashuleni na wasijenge urafiki na mtu ambaye hana msaada chanya kwenye maisha yao na kutaka kila mtu ajitambue katika nafasi yake.

"Tambua wewe ni nani, ishi katika malengo yako, hii elimu unayoipata hapa kuna mwenzako ameikosa hakikisha hupotezi nafasi kama hii," Amesema.

Kwa upande wao wanafunzi wa shule hiyo kwa pamoja waliishukuru taasisi hiyo kwa kuwapa motisha na kuwafundisha mbinu mbalimbali za kuwainua, kujiamini na kujitambua na kuahidi kusoma kwa bidii ili wasimuangushe Rais Magufuli ambaye amewekeza fedha nyingi kwenye sera ya elimu bure.