Vijana Ruagwa waipongeza serikali kwa kuwawezesha stadi za kilimo cha kisasa


Vijana Wilayani Ruagwa wameipongeza Serikali kwa kuwawezesha kupata mafunzo ya kilimo cha Kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba (Greenhouse) ambayo yamekuwa ni chachu kwao kujikwamua kiuchumi.


Pongezi hizo zimetolewa wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alipotembelea vijana hao katika Kijiji cha Chimbila “A” kilichopo Wilaya ya Ruagwa kukagua maendeleo ya mafunzo waliyopata vijana kupitia teknolojia ya Kitalu Nyumba.


Mheshimiwa Mhagama alieleza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeonesha kuwajali, kuwatambua na kuwathamini vijana kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yamekuwa yakiwasaidia sana katika kuwaendeleza vijana kulima kwa mkakati.

“Mafunzo hayo yamewajengea uwezo vijana wa kushiriki kwa wingi kwenye kilimo cha aina hii kwa kuwa kinatija na ufanisi, hivyo vijana watakuwa kupata mavuno zaidi katika eneo dogo kuliko eneo la wazi, uwezo wa kupata soko la mazao utakuwa wa uhakika, matumizi ya maji ni madogo katika kilimo hiko na hudhibiti viwatilifu,” alisema Mhagama.

Alieleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ilianzisha Programu ya Ukuzaji Ujuzi ikiwemo mafunzo hayo ya kilimo cha Kisasa ikiwa ni mkakati wa serikali baada ya kubaini asilimia 56 ya nguvukazi nchini ambao ni vijana wamekuwa na changamoto ya ajira, katika kutatua changamoto hiyo kundi hilo limewezeshwa kwa kujengewa uwezo wa kupatiwa ujuzi katika fani mbalimbali.

Waziri Mhagama aliongeza kuwa Mafunzo hayo ya kilimo kupitia teknolojia ya kitalu nyumba yatawasaidia kuboresha stadi bora za kilimo kwa vijana hususan waliopo vijijini ili waweze kujiajiri, kuajiri wenzao na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Aidha aliwasihi vijana kuendelea kutunza vitalu nyumba hivyo kwa kuwa watanufaika kiuchumi na sambamba na kuwaleta maendeleo yao na jamii kwa ujumla.

Baadhi ya vijana walionufaika na mradi huo akiwemo Bw. Lucas Mwindima alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli imeonesha dhamira ya dhati katika kuwawezesha vijana wanapata ujuzi utakaowawezesha kukuza ujuzi wao na kuwaondoa katika hali ya umaskini.

“Tunamshukuru Rais Magufuli kwa kutuwezesha vijana kupata mafunzo haya ya kilimo cha kitaalamu yaliyoleta tija tunaona uzalishaji wa mazao ulivyokua tofauti na zamani na mazao tunayozalisha yanafursa ya kupata masoko ndani au nje ya nchi,” alisema Mwindima.

Katika kupongeza jitihada hizo wanufaika wa programu ya kilimo hicho walibainisha mafanikio mbalimbali ikiwemo kupata ujuzi wa kilimo cha mazao biashara pamoja na ongezeko la ajira kwa vijana waliowezeshwa elimu hiyo.

Pia Waziri Mhagama alitembelea kikundi cha Ruangwa Materials ambacho kimenufaika na Mkopo wa Maendeleo ya Vijana unaoratibiwa na Ofisi yake kupitia Idara ya Manedleo ya Vijana.