Vikwazo 174 vya biashara EAC vyaondolewa

Jumla ya vikwazo 174 sawa na asilimia 75 vimeondolewa ili kurahisisha ufanyaji biashara kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo sasa itawezesha kuwepo kwa biashara kubwa baina ya nchi hizo.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam katika Ufunguzi wa Mkutano kati ya Wafanyabiashara na Kamati ya Taifa inayoshughulikia vikwazo vya biashara, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mtangamano wa Biashara, Bi.Sekela Mwaisela alisema kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na kanda zingine kuna sheria ambazo zinazingitia biashara.


“Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Ibara ya 13(1) Itifaki ya Umoja wa Forodha ya Biashara pamoja na Ibara ya 6 ya Itifaki ya Biashara kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi zaKusini mwa Afrika (SADC) zinazitaka Nchi Wanachama kuondoa vikwazo vya zamani ili kuwezesha biashara kwa wafanyabiashara”, Alisema Mwaisela.

Mwaisela alieleza kuwepo kwa juhudi za kuondoa kabisa vikwazo kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki zikishirikisha kuwepo kwa vikao vya kamati za biashara, Mikutano ya Kikanda, Mikutano ya Mawaziri pamoja na Mikutano ya Nchi kwa Nchi hiyo itatoa fursa kwa wafanyabiashara kutoa changamoto zao kwa utatuzi zaidi.

Katika kuteleza hilo Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na wadau leo imefungua Mkutano wa wadau wa biashara ambapo agenda kubwa ni kuelimisha wafanyabiashara kuhusu kutoa taarifa iwapo watakutana na vikwazo mbalimbali wakiwa kwenye kusafirisha bidhaa zao.

“Kusudi kubwa la Mkutano huu leo ni kujadiliana kuhusu kutoa vikwazo lakini pia kuwawezesha wafanyabiashara kuwa na elimu kuhusu hivyo vikwazo wanavyokutana navyo, sehemu gani ya kutoa taarifa kwa Msaada Zaidi”, alisema Mwaisela.

Alisema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini kwa kujenga miundombinu wezeshi ikiwemo Bandari, Reli, ambavyo vinaambana na ujenzi wa miradi mikubwa kama ule wa Reli ya Kisasa (SGR), Ujenzi wa Bwawa la kuzalisha Umeme Julias Nyerere Hydro Power Poject (JN HPP) ambao utazalisha Megawati 2,115.

Kwa upande wa wadau wa biashara wao wamesema kuwa Serikali imewezesha kuwepo kwa mazingira mazuri ya biashara katika Jumuiya ya Nchi wanachama ukiachilia mbali kuwepo kwa vikwazo vidogovidogo ambavyo vinatatulika.

“Mkutano huu unaonesha nia njema ya Serikali kuweza kuwasiliana kwa karibu na wafanyabiashara ili kuweza kujua changamoto zao na mazingira ya biashara wanayokutana nayo sokoni, tumefurahi kwamba Serikali imejitahidi kupunguza changamoto za biashara” David Minja, Unilever.