Mkuu wa wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga, Kissa Gwakisa amewaonya waandikishaji na waandaaji wa orodha ya wapiga kura wilayani humo watakaobainika kuwaingiza raia wa kigeni kwamba hawatasalimika badala yake watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
DC Kissa aliyasema hayo wakati akifungua mafunzo kwa waandikishaji na waandaaji wa orodha ya wapiga kuwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 ambapo aliwataka wawe makini ili wasijikute wameingia matatani.
Alisema kwamba pamoja na kuwepo kwa mafunzo hayo lakini wapo baadhi ya waandikishaji na waandaaji wa orodha ya wapiga kura kwenye uchaguzi huo wanaweza kufanya tofauti na maelekezo hivyo watahakikisha wanashughulikiwa kwa mujibu wa sheria zilizopo.
“Ndugu zangu wasimamizi uchaguzi wilayani, wanasimamia uchaguzi wasaidizi ngazi ya wilaya, Kata, Vijini na Mitaa kuhakikisha wanakuwa waaminifu na nidhamu wakati wa kutekeleza majukumu yenu na hii itasaidia kuepusha malalamiko huku akiwaonya watakaokwenda kunyume watachukuliwa hatua kali dhidi yao “Alisema DC Korogwe.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wasimamizi hao kuwa mfano mzuri katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuhakikisha wanatenda haki ili uchaguzi uweze kwenda kwa haki na usalama bila kuwepo na malalamiko ya aina yoyote ile.
“Lakini pia niwaambie kwamba elimu hii muende kuitoa na ngazi za chini..kupiga kura ni haki ya kila mtanzania hivyo tunawategemea kama Taifa kundi hili lipo kila kila wilaya kwa nyie wa hapa nataka kuona mfano mzuri Korogwe Uchaguzi uende vizuri kusiwe na malalamiko”Alisema DC Kissa.
