Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amepongeza vijana kwa kuonesha niya njema ya kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa sambamba na kuendeleza mambo mema yote aliyoyafanya enzi za uhai wake.
Ameyasema hayo wakati wa hafla ya kuwaaga vijana 60 waliopanda Mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kuadhimisha kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika Marangu, Mkoani Kilimanjaro.
Waziri Mhagama alisema kuwa, Baba wa Taifa Mwl. Julius K. Nyerere alikuwa kiongozi mzalendo kwa nchi yake na aliyejali utu na usawa, hivyo ni jambo zuri kuona vijana wakiendelea kuenzi falsafa za mhasisi wa Taifa hili Mwl. J. K. Nyerere pamoja na Hayati Mzee Abeid Aman Karume ambao kwa kiasi kikubwa wamechangia katika suala zima la kudumisha umoja na msikamano wa Taifa.
“Kitendo hiki wanachofanya vijana kwa kupanda mlima Kilimanjaro ni jambo la kishujaa na uzalendo wa hali ya juu kwa Taifa ni matumaini yangu vijana wengi wataiga mfano huu mzuri,” alisema Mhagama
Alieleza kuwa, Baba wa Taifa Mwl. Julius K. Nyerere alifanya kazi kubwa ya kujenga misingi imara ya nchi kuwa na amani, umoja, mshikamano pamoja na misingi ya kuwa na uchumi wa kujitegemea.
“Vijana mnatakiwa kuendeleza na kuiga utendaji kazi wa Baba wa Taifa Mwl. Julius K. Nyerere alijitolea kwa mambo mengi ili kujenga Taifa, alikuwa mstari wa mbele katika kupambana na mambo mengi ikiwemo ujinga, maradhi na umaskini ili kila mtanzania awe na maisha bora. Hiyo ilikuwa ni ishara tosha kwa vijana kutambua namna Baba wa Taifa alivyolipigania nchi yetu,” alisema Mhagama
Aliongeza kuwa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Dkt. Alli Mohammed Shein ni mfano tosha wa kuigwa na vijana, wanaonesha namna wanavyojitoa kwa ajili ya Taifa na kuhudumia wananchi pamoja na kukuza uchumi wa nchi.
Waziri Mhagama alifafanua kuwa, kuelekea kilele cha mbio za mwenge mwaka huu vijana hao waliopanda mlima Kilimanjaro watapata fursa ya kujumuika na vijana kutoka kwenye nchi jirani ikiwemo Angola, Zimbabwe, Msumbiji, Afrika Kusini, Uganda, Rwanda na Kenya katika kongamano la kujadili mchango wa Baba wa Taifa barani Afrika.
Aidha Waziri Mhagama alitoa wito kwa watanzania wote hususan vijana kuendelea kuenzi falsafa za waasisi wa taifa hili Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mzee Abeid Aman Karume kwa kutambua kuwa waasisi hao ni urithi tosha. Pia aliwasihii vijana kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuyaenzi yaliyofanywa na waasisi hao.

