Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imeeleza kuwa wamewasilisha barua yao yenye maelezo kuhusu mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa ndani ya Chama unaoendelea katika ngazi mbalimbali nchini ambapo hitimisho lake litakuwa ni uchaguzi ngazi ya Taifa utakaofanyika, Disemba mwaka huu.
Barua hiyo yenye kurasa 13 na viambatanisho 8, imewasilishwa leo Jumatatu Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, jijini Dodoma, saa 3 asubuhi na ofisi hiyo imethibitisha kupokea barua hiyo kwa kusaini 'dispatch'.
Kupitia barua hiyo, Chadema kimemthibitishia Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuwa, Chama kinaendelea kutekeleza shughuli zake, ikiwa ni pamoja na Uchaguzi Mkuu wa ndani kwa kuzingatia taratibu za kisheria, Katiba ya Chama na Kanuni za Uendeshaji wa Chama.

