Na John Walter, Manyara
Imeelezwa kuwa wanariadha ni Mabalozi wazuri wa kuutangaza Utalii wa mkoa wa Manyara, kwa kuwa kupitia mashindano ya michezo hiyo huwa wanatembelea mikoa mbalimbali ya nchi na wengine huenda hadi nje ya nchi na yote hiyo ni fursa kubwa ya kuutangaza Utalii.
Hayo yamesemwa na Mhifadhi mkuu wa Tarangire Ignas Gara wakati akiongea na wanariadha walioitembelea hifadhi hiyo, baada ya kushiriki mbio za kilomita 10, 5, na 2.5 mjini Babati tarehe 21 Septemba 2019 zilizoandaliwa na klabu ya Garmaa yenye makao yake mjini hapo.
Wanariadha waliopata fursa ya kutembelea hifadhi hiyo ya Tarangire, ambao pia ndiyo waliokuwa wafadhili wakuu wa mbio hizo ni wale walioshindana na kushika nafasi ya kwanza hadi ya tatu Me na Ke kwa kila mbio.
“Wanariadha ni watu wanaotembea nchi mbalimbali hivyo ni rahisi kutumika kuutangaza Utalii wetu kwa watu wanaokutana nao hivyo kutuletea fedha za kigeni,hivyo tunawashauri washirikine na sisi pale wanapopata fursa za kwenda nje kwa wale wanaoshiriki mbio za kimataifa” alisema Gara.
Alieleza kuwa michezo inaweza ikatumika kupata watalii wa ndani na vilevile watalii wanaoingia kutoka nje kwa kuitangaza nchi yetu ya Tanzania pamoja na vivutio vya Utalii vilivyoko pia wawasiliane na Taasisi zinazotangaza Utalii.
