Watu 100 wafariki katika maandamano Iraq

Takriban watu 100 wamepoteza maisha, katika maandamano ya kupinga serikali nchini Iraq. Vifo hivyo, vimetokana na makabiliano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama.

Tangu siku ya Jumanne, maelfu ya watu wameingia barabarani nchini humo na kuandamana kupinga rushwa, ukosefu wa ajira, maji safi na huduma mbovu hasa za umeme.

Watu wanne walikufa kwenye maandamano hayo hapo jana Jumamosi wakati maafisa wa usalama walipowafyatulia waandamanaji wapatao 200 waliokuwa wamekusanyika katika mji mkuu Baghdad.

 Maandamano ya Iraq ambayo kwa kiasi kikubwa yanaongozwa na vijana yaliibuka tena mwishoni mwa wiki baada ya amri ya kutotoka nje kuondolewa mjini Baghdad, mapema siku ya Jumamosi.