Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliyemaliza muda wake Prof. Mussa Assad, amesema baada ya kukabidhi ofisi kwa CAG mpya Charles Kichere, kazi pekee atakayoifanya kwa sasa ni kuwa Mkulima.
Ameeleza hayo leo wakati akimkabidhi ofisi CAG mpya Charles Kichere, ambapo amesema licha ya changamoto alizopitia bado atampa ushirikiano wakutosha Charles Kichere.
"Baada ya hapa mimi nitafanya kazi ya kulima kwa sababu miezi miwili iliyopita nilianza kuwekeza kwenye kulima, kwa hiyo wakinihitaji watu wa Mjini nitakuja, kuhusu changamoto ni nyingi nimepitia mnataka niseme hapa nitatia ukakasi hakuna haja ya kutia ukakasi." amesema.
"Kazi ya CAG ni kusaini ripoti lakini ripoti unachukua kazi za watu wengi sana ambao waliifanya maeneo mbalimbali hapa Tanzania, kwa hiyo nukta yangu ni kuwatazama vizuri sana watu hawa." ameongeza Prof. Assad.
Ikumbukwe Novemba 03, 2019 Rais John Magufuli alitangaza kumteua Charles Kichere kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), baada ya Prof. Mussa Assad kufikia tamati Novemba 04 mwaka huu.
