China yaja mkakati wa kupambana na vitendo vya ujangili Hifadhi ya Taifa ya Mikumi

Ubalozi wa China nchini Tanzania  umeunga  juhudi za Serikali ya Tanzania katika  mapambano dhidi ya  ujangili kwa kuziwezesha jamii zinazoishi karibu na Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kwa kuzipa  pembejeo za kilimo ikiwa pamoja na  kuzijengea uwezo wa kulima kisasa ili kuwasaidia wananchi hao kuacha kujihusisha na vitendo vya ujangili.

Hayo yamebainishwa leo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu wakati Ubalozi wa China nchini ukikabidhi msaada wa pembejeo za kilimo kwa  wananchi wa kijiji cha Mhenda katika wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.

Ubalozi wa China nchini Tanzania umetoa msaada wa mbegu  za mahindi yenye  ujazo wa kilo 2500, mbegu za alizeti  zenye ujazo wa kilo  150 pamoja  mbegu za choroko zenye ujazo wa kilo 800
Mbali na msaada huo, Ubalozi huo umetoa jumla ya jozi 13 za sare za ulinzi shirikishi, buti 13, komputa mpakato nne pamoja runinga moja.


Mhe.Kanyasu amesema lengo la vifaa hivyo ni kuwasaidia wananchi kujikita katika kilimo cha kisasa kwa kutumia mbegu zenye ubora wa hali ya juu.

Akizungumza katika mkutano huo, Mhe. Kanyasu amesema  vifaa hivyo vitatumika katika kutoa elimu kwa wananchi katika mapambano dhidi ya vitendo vya ujangili.

Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu ameipongeza Jamhuri ya watu wa China kukomesha soko la meno ya tembo na kuamua kutoa msaada kwa wanavijiji ili nao waweze kuachana na biashara hiyo haramu.

Awali, Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke amesema pembejeo za kilimo walizozitoa itakwenda sambamba na mafunzo yatakayotolewa na wataalam kutoka China watakaowafundisha wanakijiji kulima kwa kisasa ili waweze kuachana na vitendo vya ujangili.

Ameeleza kuwa Ubalozi wa China umeamua kuanza na kijiji hicho ili kuwasaidia wananchi kuweza kuzalisha mazao mengi ili wasiweze kujiingiza katika vitendo vya ujangili.

Amesema China imeamua kuisaidia Tanzania katika mapambano ya vita dhidi ya ujangilli kwa vile watalii wanakuja nchini kwa ajili ya kuangalia wanyama, hivyo vitendo vya ujangili vinakwamisha juhudi za serikali katika kujiletea maendeleo.

Aidha, Balozi huyo ameipongeza Taasisi ya  Kova SUKOS Foundation inayoshughulikia majanga kwa kuratibu tukio hilo ikiwa pamoja na  kujitoa kuhakikisha wananchi wa Mhende wanakabidhiwa misaada hiyo itakayowasaidia katika kujiondoa katika umasikini huku utalii ukizidi kushamiri.

Naye Diwani wa kata ya Mhenda, Ali Athumani amemshukuru Balozi wa China kwa msaada huo na kuahidi kuwa watakuwa mabalozi kwa vijiji vingine vilivyo karibu na Hifadhi hiyo.