Kali ya mwaka kutoka kwa mwanasiasa wa India

Huko nchini India mwenyekiti wa chama cha siasa cha BJP wa eneo la  Bengal ya magharibi, ndugu  Dilip Gghosh, amedai kwamba maziwa ya ng’ombe wa India yana dhahabu na kwa yeyote atakayekunywa maziwa hayo atapata afya na utajiri.

Gghosh akizungumza katika mkutano wa wazi wa chama hicho cha BJP alitetea madai yake hayo kwa kusema kwamba tofauti ya ng’ombe wa maeneo mengine na wale wa India ni kwamba ng’ombe wa India wana mshipa wa damu maalumu ambao wengine hawana.

Gghosh aliendelea kusema kwamba mshipa huo maalumu unapopigwa na miale ya jua huwezesha kutengenezeka dhahabu katika maziwa na hivyo kwa wote watakaokunywa maziwa hayo watapata afya na kuwa matajiri. Kwa minajili hiyo ng’ombe hao ni budi walindwe.

Mwanasiasa huyo wa BJP aliendelea kusema kwamba ng’ombe wanaoletwa nchini humo kutoka mataifa mengine sio ng’ombe bali ni kama madudu.

"Hao sio ng’ombe zetu mama, ni shangazi zetu. Kuwaabudia shangazi zetu hakutaleta jema lolote kwa nchi” alisema mwanasiasa huyo.

Maelezo ya Gghosh yamekuwa ndio habari inayozungumziwa zaidi katika mitandoo ya kijamii, Huku wanasiasa wengi wakisema maelezo hayo ni ya kijinga. Na weengine wakisema maelezo hayo ni kituko na wengine wakiyapinga.