Mambo yatakayokufanya uendelee kuwa maskini wa kipato


Kati ya kitu ambacho unatakiwa kuwa makini nacho kila mara wakati unatafuta mafanikio, ni yale mambo unayoyafanya kila siku. Mambo hayo unayoyafanya ndiyo ambayo yanaweza kukupa picha utafanikiwa au hutafanikiwa katika maisha yako endapo utayafatilia kwa makini.

Kimsingi, yapo mambo ikiwemo tabia zako ambazo ukizifanya ni lazima ufanikiwe. Pia kwa upande mwingine yapo mambo, ambayo ukiyafanya iwe kwa kujua au kutokua ni lazima uwe maskini. Kwa kusoma makala haya itakusaidia kuelewa mambo ambayo ukiyafanya kila wakati ni lazima uwe maskini utake au usitake.

Fuatana nami katika makala haya kujifunza mambo hayo:-

1. Fanya kazi chini ya saa kumi kila siku.
Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya mafanikio, ili uweze kufanikiwa unahitaji kufanya kazi kwa saa zisipongua kumi kila siku. Ikiwa utakuwa unafanya kazi kwa saa nane, basi utaishia kuwa na maisha ya kawaida ambayo kila mtu anayo. Maisha makubwa ya mafanikio yanakuja kwa kujituma na kufanya kazi kwa muda mrefu.

Historia inaonyesha wengi kati ya watu wenye mafanikio makubwa duniani, wanajituma na kufanya kazi kwa saa zaidi ya kumi kwa siku. Kwa mfano, Thomas Edson mgunduzi wa taa za umeme ilifika wakati alifanya kazi hadi kwa saa 18 kwa siku. Jiulize unafanya kazi zako binafsi kwa saa ngapi? Kama unafanya chini ya saa kumi, jiandae kuwa maskini.

2. Fanya kazi chini ya siku sita kwa juma.
Mbali na kufanya kazi chini ya saa kumi kwa siku, pia unatakiwa kufanya kazi kwa siku zisizopunguaa sita kwa wiki. Hapa tunapozungumzia kazi, namaanisha kazi zako binfsi na si kazi ya kuajiriwa. Ila kama unafanya kazi zako chini ya siku sita basi, andika maumivu ni lazima utakuwa maskini utake au usitake, hilo ni lazima.

3. Angalia televisheni kila siku kwa muda unaozidi saa moja.
Kitu kimojawapo ambacho kitakufanya uwe maskini ni kuangalia televisheni kwa muda mrefu. Wapo watu ambao ni kama walevi wa TV. Kila siku hupoteza muda mwingi sana kwenye TV kuliko kawaida. Unapotumia muda mwingi kwenye TV na kusahau kwamba ungeweza hata kujisomea na kuboresha maisha yako, basi jiandae pia kufa maskini.

4. Kuwa mlevi wa mitandao ya kijamii.
Kama wewe unatumia muda wako mwingi sana kuingia kwenye mitandao ya kijamii kama facebook, twitter au instagram zaidi ya saa mbili kwa siku, basi naweza sema tayari umeshajiandikisha kwenye daftari la kuelekea kwenye umaskini. Hautaweza kukwepa kuwa maskini ikiwa matumizi yako ya muda ni mabovu kiasi hicho tena kwa mambo yasiyo ya msingi.

5. Kuwa mtu wa matumizi.
Kati ya shimo ambalo wengi wanatumbukia bila kujijua na kupelekea wao kuwa maskini ni kwa wao kuwa watu wa matumizi na kusahau kuwekeza. Kiasi chochote cha pesa unachopata, unashauriwa kuwekeza kidogo kwanza. Kama haufanyi hivyo na unaponda mali tu,  basi elewa upo kwenye njia ya kuelekea kwenye umaskini.

6. Usijifunze kitu.
Wakati wenzako wanawekeza kwenye maarifa, wewe tulia tu hapo ulipo usijifunze, ni lazima uwe maskini. Kama ni soga endelea kuzipiga tu bila kuchoka. Wengi wanakufa maskini kwa sababu ya kuamua kwa makusudi kutokujifunza iwe kupitia vitabu au kujifunza kupitia maisha ya watu wengine hususani wale waliofanikiwa.

Kwa kifupi, hayo ndiyo mambo ambayo ukiyafanya yanauwezo mkubwa wa kukufanya ukawa maskini utake au sitake.