Mateso kwa mtoto, yafanya wazazi kurejesha mahari


Mtendaji wa Kijiji cha Mpwayungu Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Selemani Kibakaya amesema wazazi wawili waliowaoza binti zao wenye umri wa miaka 14 wamekubali kurejesha fedha na mifugo waliyopokea kama mahari .

Uamuzi huo umetokana na wazazi hao kubaini kuwa watoto wao wamekuwa wakiteseka kwenye ndoa zao.

Akizungumza wakati wa mahojiano baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Shirika Lisilokuwa la kiserikali la Woman Wake Up (Wowap) ambalo linatekeleza mradi wa Sauti Yangu, Kibakaya alisema wazazi sasa wanabadilika kutokana na elimu inayotolewa.

"Sasa wazazi wana uthubutu wa kufika kwenye ofisi za kijiji baada ya kugundua kuwa walifanya makosa kuwaoza mabinti katika umri mdogo," alisema.

Alisema walifanya utafiti wakagundua mila za kabila la Wagogo binti akivunja ungo anaweza kuolewa na kijana wa kiume anapobalehe anaweza kuoa na wanaoza watoto bila kuangalia umri. Kibakaya alisema mkazi mmoja wa Nagulo alimuoza binti mwenye umri wa miaka 14.

Binti huyo akaishi miaka mitatu ndani ya ndoa akiwa mpweke kwani kijana aliyemuoa aliondoka muda mrefu na kwenda Dar es Salaam kutafuta maisha. Alisema wazazi wa binti walifika ofisi za kijiji na kutaka ufanyike utaratibu wa kurudisha mahari ili waweze kuondoka na binti yao.

"Tulikaa kikao cha pamoja baina ya wazazi na tukapitisha maamuzi mahari irudishwe ambayo ilikuwa ni fedha taslimu Sh 400,000, mbuzi watatu na magunia matatu ya mtama, wazazi wakarudisha mahari na binti yuko kwa wazazi wake," alisema.

Pia alisema binti mwingine wa kijiji hicho aliolewa akiwa na miaka 14 akaishi na mwanaume ambaye baadae alienda mkoani Mbeya kutafuta maisha.

"Wazazi walikiri kufanya makosa kumuoza binti yao, wakakubali kurudisha mahari ambapo ni fedha taslimu Sh 150,000, mbuzi moja, na gunia mbili za mtama na binti yuko mikononi mwa wazazi wake,"alisema.

Alisema binti huyo ana mtoto moja na wamekubaliana kila mwezi zitolewe Sh 35,000 na madebe matatu ya mtama kama gharama za matunzo ya mtoto.

"Kama wazazi wameanza kuona mateso wanayopata watoto wanaoolewa katika umri mdogo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuibadilisha jamii," alisema.

Mradi wa Sauti yangu umedhamiria kuimarisha uwezo na ushiriki wa watoto katika kushughulikia vitendo vya ukatili kwa watoto na vile vinavyoshusha ufaulu wao katika masomo. Mradi huo unafadhiliwa na Shirika la Child Fund Korea kupitia Jukwaa la Haki za watoto.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items