Loading...

11/29/2019

Moto wawaka chini ya ardhi kwa miezi minne NjombeNa Amiri kilagalila-Njombe

Wananchi wa mtaa wa mji mwema kata ya mji mwema halmashauri ya mji wa Njombe mkoani humo wameshikwa na butwaa na kitendo cha moto kuwaka chini ya ardhi kwa takribani miezi minne katika mtaa huo,huku baadhi ya wakazi wa mtaa huo na maeneo jirani wakifika katika eneo hilo kwa ajili ya kuona maajabu hayo.

Kwa mujibu wa maelezo ya mashuhuda wamedai moto huo uliibuka mwishoni mwa mwezi August na umekuwa ukikolea taratibu kuelekea chini ya ardhi huku ukifuka moshi na kutengeneza majivu juu na kusababisha shimo ambalo kasi ya kuongezeka kwake imekuwa ikiongezeka.


Baadhi ya wakazi wa mtaa mji mwema wanaoishi jirani na eneo linaloungua akiwemo Elisha John na Andrea Msemwa wamesema wametumia kila njia kuzima moto huo hata kwa kutumia maji pamoja na mvua kubwa zinazoendelea mkoani hapa lakini imekuwa ngumu kuzima moto huo.

“Watu wote tunakuja kushangaa moto unazidi kuwaka lakini hatuelewi ni kwanini unawake kwa kuendelea kushuka chini au kuna madini hatuelewi na moto wenyewe unatengeneza asili ya majivu,ni hali ya kushangaza kwa kweli sio kitu cha kawaida unaweza kukaa hapa kumbe chini kumeshaungua”Alisema Elisha John.

Mzee John Changula ni mmoja wa wananchi hufanya shughuli zake ikiwemo kilimo katika eneo hilo linalomilikiwa na taasisi ya shule ya viziwi Njombe anasema awali alichoma mabua lakini aliporudi shambani baada ya wiki tatu alikuta ardhi ikifuka moshi hali ambayo imezidi kuwa mbaya hadi sasa huku mchungaji Alfonce Ngavatula mkurugenzi wa taasisi hiyo akiomba mamlaka za serikali ikiwemo zima moto na madini kufanya uchunguzi zaidi pamoja na kuzima moto huo.

“Kwanza nililima hili shamba nikawa nimekusanya mabua na kuyachoma moto,kuzima kwenyewe nikawa nachota maji nakuja namwaga,sehemu nyingine nilifanikiwa kumaliza kweli kuzima moto lakini hapa ulinishinda”Alisema John Chagula

“Wataalamu wanaohusika na maswala ya madini na udongo wakifika eneo hilo wanaweza kuangalia udongo na wanaweza kusema ni kweli ni maozea”alisema Mchungaji Alfonce Ngavatula.

Kufuatia hali hiyo timu ya wataalamu ya mkoa wa Njombe ikongozwa na Wilfred Machumu inalazimika kufunga safari mpaka eneo la viziwi linaloungua ili kujua kiini cha kuibuka kwa moto huo na kueleza sababu za kitaalamu zinazoweza kupelekea ardhi kuungua endapo kutakuwa na uozo wa miti,Makaa ya mawe pamoja na uwepo wa mafuta.

“Hili tutalifanyia kazi kuanzia kesho tutafuta vifaa vya kuchimbia hapa tuone chini kuna nini,tukishajua kuna nini kinachofuatia ni kuhakikisha huu moshi hauendelei,nilishawahi kufanya kazi kama hii huko Songea sehemu moja inaitwa Mbuyula mkaa nao ulikuwa kama hivi hivi lakini hatua ya kwanza tulijiridhisha kwamba ni mkaa ndio unawake?”alisema Wilfred Machumu

Moto huo ambao umewaka kwa zaidi ya miezi minne umeibua hisia tofauti kwa wananchi hatua ambayo imefanya idara ya madini kuchukua sampuli ili kwenda kuchunguza zaidi ikiwa ni pamoja na kutafuta njia ya kuuzima.
KWA HABARI, LIVE TV, RADIO, MATOKEO YA LIGI ZOTE DUNIANI DOWNLOAD APP YA MUUNGWANA BLOG <DOWNLOAD HAPA>
Share:
Loading...
Loading...

Popular Posts

Copyright © MUUNGWANA BLOG | Powered by Blogger