Naibu Waziri amfukuza eneo la kazi Bosi wa TBS


Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara nchini Tanzania, Stella Manyanya amemwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwanda nchini humo (TBS) kumwamisha kituo cha kazi aliyekuwa kaimu msimamizi wa TBS kituo cha Namanga, Martha Suda  kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake katika utendaji kazi.

Ameyasema hayo wakati akizungumza katika kituo cha ofisi hiyo kilichopo Namanga wakati alipofanya ziara yake ya kikazi.

"Nilitoa maagizo hayo muda mrefu lakini leo nimekuja hapa nashangaa hayo maagizo hayajatekelezwa na sijui kwa nini, sasa Serikali hii haina mchezo na haipo tayari kukaa na kufanya kazi na watu wazembe kama hawa.”

“Tunaomba huyu Martha ahamishwe kituo kingine cha kazi haraka iwezekanavyo na nitafuatilia hilo," amesema Injinia Manyanya.

Manyanya amesema kwa sasa hivi nafasi hiyo itashikiliwa na Peter Musiba ambapo alimtaka kufuata sheria na kanuni huku akiwataka kuondokana na uzembe ambao umekuwa ukifanyika kituoni hapo.