Serikali kutoa Milioni 300 kwaajili ya mradi wa kusambazia Maji wananchi


Serikali imeahidi  kutoa milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa usambazaji wa maji kwa wananchi kutoka chanzo cha maji cha Tura wilayani Uyui ili  kuwaondolea kero ya upatikanaji wa maji ya uhakika ya muda mrefu kwa wakazi wa eneo hilo.

Fedha hizo ni sehemu zitakazotumika katika kukamilisha mradi huo ndani ya kipindi cha miezi mitatu.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa wakati wa ziara yake Wilayani Uyui Mkoani Tabora kwa ajili ya kutatua kero za maji kwa wananchi wa eneo hilo.

Alisema kukamilika kwa chanzo hicho cha maji kitasaidia kuzalisha lita zaidi ya milioni 2.7 na kuwahudumia wakazi zaidi ya 11,000 na hivyo kuwaondolea usumbufu wa kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

Alisema kuwa Serikali haiwezi kuona wananchi wanateseka kutafuta maji kwa umbali mrefu huku kukikwa na chanzo cha maji kizuri ambacho hakitumiki.

Waziri huyo alisema mradi huo utakuwa na hatua tatu ambazo ni ujenzi wa kituo cha kutoa maji kwenye bwawa na kusafisha maji, hatua ya pili ni ujenzi wa tenki  la  upokeaji wa  maji na hatua ya mwisho ni ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa maji kwa wananchi.

Naye Mbunge wa Jimbo Igalula Mussa Ntimizi alisema kuwa licha ya bwawa hilo kumilikiwa na Shirika la Reli Tanzania(TRL) wamekubaliwa lianze kutumika kutatua kero ya maji kwa wananchi