Serikali kutumia wataalamu wa ndani kutekeleza miradi


 Ezekiel Mtonyole-Mpwapwa

Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa, amesema wamekusudia kuanzia Sasa kuanzisha utaratibu wa kutokutumia wakandarasi au kutoa tenda katika miradi ya maji inayotekelezwa maeneo mbalimbali hapa nchini na badala yake watatumia wataalamu wa ndani ya Mamlaka za maji kukamilisha miradi hiyo.

Waziri Mbarawa ametoa kauli hiyo  Wilayani Mpwapwa wakati wa ziara yake kukagua  utekelezaji wa miradi ya Maji, ambapo amesema wamefikia hatua hiyo baada ya wakandarasi wengi kuchukua fedha na kutokukamilisha miradi hiyo, amesema serikali imewekeza fedha nyingi Sana lakini matokeo yake hayaonakani.

Na kubainisha kuwa miradi mingi wanapewa wakandarasi ambao hawana uwezo au kupeana tenda kindugu na kutekeleza miradi chini ya kiwango.

"Serikali za awamu zote zilizopita ilitenga fedha nyingi Sana kwa ajili ya miradi ya maji lakini matokeo yake hayaonekani wote tunajiuliza fedha zinakwenda wapi wakati maji hayatoki na fedha hazirudishwi na majibu yake kila mtu anayo" amesema.

"Kwahiyo tumeamua kuja na utaratibu huu wa kutowatumia wakandarasi na badala yake tutatumia wataalamu wa ndani ya Mamlaka zetu za maji na mfano tumefanya hivyo Mkoa wa Katavi na matokeo tumepata" amesema Waziri Mbarawa.

Katika Ziara hiyo Wilayani Mpwapwa ametembelea miradi ya maji Luhundwa na Bumila kuona utekelezaji wake wake na akiwa katika mradi wa Maji wa Bumila, Waziri wa Mbarawa amewahakikishia wananchi wa Kata hiyo kuwa hivi karibuni wataanza kupata huduma ya maji Safi.

Kwani mradi huo ulikwama kutokana na mkandarasi kutolipwa fedha lakini kwa Sasa mkandarasi huyo kashalipwa fedha na mradi huo utakamilika ndani ya mda mfupi na wataanza kupata huduma ya maji.


Awali Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Jabir Shekimweri akitoa taarifa ya Mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt Binilith Mahenge, amesema licha ya miradi mingi kutokukamilika lakini bado huduma ya maji inazidi kuimarika kwani mwaka 2015 ni asilimia 43 tu ndio walikuwa wakipata huduma ya maji na Sasa ni asilimia 57 kwa miji midogo na Wilaya.

Wakati kwa miji mikubwa upatikanaji wa maji ilikuwa, ni  asilimia 65 na Sasa ni asilimia 82, na wamejipanga angalau kufikia mwaka 2025 kwa miji midogo ifikie asilimia 80 na miji mikubwa wafikie asilimia 95.

Baadhi ya Wananchi wa wanaozunguka mradi wa Maji wa  Bumila  wameishukuru serikali kwa kuleta fedha za mradi huo kwani shida ya maji katika eneo hilo ni kubwa sana. Wamesema angalau Sasa adha ya maji itapungua kwa kiasi kikubwa Sana kwani hiyo ilikuwa kero kubwa  kwao.