Polisi Wilayani Ibanda nchini Uganda Ibanda wamevikuta vichwa viwili vya binadamu (Mwanaume na Mwanamke) vikiwa vimetupwa shambani maeneo ya Kyegwisa ambapo ni kilomita tatu kutoka Ibanda mjini.
Katika uchunguzi wa awali, Polisi wamewaeleza waandishi wa habari kuwa mauaji hayo yatakuwa yalifanyika mbali na eneo ambalo vichwa hivyo vimeokotwa. Hata hivyo, Polisi na watu waliojitokeza katika kushuhudia tukio hilo hawakuweza kuvitambua vichwa hivyo ni vya kina nani.
Aidha, tukio hili limetokea baada ya siku kadhaa kupita tangu miili miwili ya mwanaume na mwanamke isiyo na vichwa kukutwa katika msitu wa Kikoyo uliopo Buhanda karibu na wilaya ya Kitagwenda ambapo kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa Wilaya Bw. Geofrey Mucunguzi anasema miili hiyo haikutambuliwa ni ya nani.
Zaidi ya hayo, Mucunguzi alisema kuwa watafanya vipimo vya DNA vya miili na vichwa hivyo ili kujiridisha kama vichwa vilivyopatikana Ibanda ni vya miili hiyo au la.
