Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala, amesema kuwa upinzani wa kuiondoa CCM madarakani bado haujazaliwa na kwamba chama hicho kitapata ushindi wa asilimia 100 katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24.
Kilakala alitoa kauli hiyo Dar es Salaam wakati akifanya mahojiano kwenye kipindi cha ‘Zungumza’ kinachorushwa na kituo cha runinga cha Clouds Plus.
Alisema kuwa kwa kazi inayofanywa na CCM chini ya Mwenyekiti wake, Rais Dk. John Magufuli ni ngumu kuwashawishi wananchi kutokuichagua.
“Sasa hivi kilichopo ni kwamba hakuna mpinzani ambaye anashindana na CCM, badala yake watasalia kuwa nafasi ya pili tu, kwani malengo yao ni kutaka kupata ruzuku tu kwa kuwa wanapata idadi ya wabunge.
“Upinzani kwa miaka hii ya sasa, 100 au 200 ndiyo wafikirie kuchukua dola, lakini siyo sasa hivi, sababu chama chetu kina mtandao mkubwa wa viongozi unaoanzia chini, huku ukishirikisha wananchi katika suala zima la maendeleo, hivyo mbadala wa CCM Tanzania bado haupo,” alisema Kilakala.
Aliongeza kuwa wapinzani wa kweli lazima watatokea CCM kwa kuwa wapinzani wa sasa bado hawajaandaa mtu wa kuja kuwa kiongozi wa Serikali.
“Mfano uchaguzi wa mwaka 2015 naweza kusema kuwa ni kama CCM wenyewe tulikuwa tunashindana, kwa sababu mpinzani mkuu wa pili alikuwa ni Edward Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu aliyelelewa na kukulia ndani ya CCM.
