Wadau wa kilimo watoa ushauri kwa Serikali


Na. Ezekiel Mtonyole, Chamwino

Serikali imeshauriwa kuwapa mfunzo ya mara kwa mara maafisa ugani ili kuwajengea uwezo wa kuwafundisha na kuwasaidia wakulima namna bora ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotokana na mabadiliko ya mifumo ya kilimo hapa nchini.

Wakizungumza wakati wa maonyesho maalumu ya mbegu na vyakula asilia yaliyofanyika Wilayani Chamwino, Mkoani Dodoma, baadhi ya wakulima wadogo wadogo walisema changamoto hizo ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, matumizi bora ya mbegu, mbolea pamoja na janga la uchakavu wa udongo.

Akiongea kwa niaba ya wakulima hao  Mwenyekiti wa   Jukwaa la Wakulima wadogo wilayani Chamwino  (JUWACHA)  Mkoani Dodoma  chini ya ufadhi wa Shrika lisilo la Kiserikali Action Aid Janeth Nyamayahasi amesema  Maofisa Ugani wanashindwa kutoa elimu ya kutosha pamoja na  matumizi bora ya ardhi na mbegu bora kutokana na ukosefu wa mafunzo ya  mara kwa mara.

"Kuna haja ya serikali kuona namna ya kuwapa elimu wataalamu wa kilimo, hasa kipindi hiki mabadiliko ya tabia ya nchi na kuwajengea uwezo wakulima namna ya kukabiliana na changamoto hiyo" amesema Janeth.

Akiendelea kufafanua amesema maofisa ugani wengi  wanashindwa kutekeleza  majukumu yao ipasavyo kwa madai yakukwamishwa madaraka kama  maafisa ardhi.

Hata hivyo amesema miongoni mwa Changamoto zinazowakabili wakulima ni pamoja na uhaba wa pembejeo na  zikipatikana zinachelewa kufika  kwa wakati, ukosefu wa masoko ya uhakika na uhaba pia wa maofisa ugani.

Licha ya hayo yote, amelipongeza Shirika la Action Aid kwa kuwa mstari wa mbele katika jitihada za kuwawezesha wakulima wanawake wadogowadogo vijijini kulima kwa kufuata kanuni za kitaalamu na kuwajendea uwezo wa kuweza kumiliki ardhi.

Kwa upande wake, Mratibu wa Shirika la PELUM Tanzania, Donati Senzia, amesema lengo la maonyesho  hayo ni kuhamasisha jamii juu ya matumizi ya chakula cha asili,kuhamasisha jamii kuendeleza mfumo wa mbegu za asili na kuwakutanisha wakulima na wataalamu wa mbegu.

Taasisi na mashirika mengine yaliyoshiriki katika maonesho hayo ni pamoja na  Wakala wa Mbegu Tanzania (ASA), Kituo cha Tafiti za Kilimo Tanzania (TARI), AGRA na  RIPAT.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items