Watumishi wa afya watakiwa kufuata miongozo ili kudhibiti maambukizi


Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Yudas Ndugile amewataka watumishi wa afya wa mkoa huo kuzingatia namna ya kufuata miongozo na taratibu za namna kukinga na kudhibiti maambukizi (IPC Standards) kipindi wanapotoa huduma kwa wagonjwa.

Dkt. Yudas amesema hayo wakati alitembelea na kufungua mafunzo yanayoendelea kutolewa na wataalamu kutoka Wizara ya Afya kwa watumishi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Halmashauri na vituo vya afya vilivyoko jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia mafunzo hayo Dkt. Yudas ameishukuru Wizara ya afya kwa kuwawezesha kuwajengea uwezo watumishi hao kufuata miongozo ya utoaji wa huduma za afya katika maeneo yao ya kazi.

“Naishukuru Wizara ya Afya kwa kuendelea kutoa mafunzo haya kwa watumishi mbalimbali wa kada ya afya nchini, hii itasaidia kuongeza ufanisi kwa watumishi wetu katika utoaji wa huduma endapo watafuatilia kwa makini miongozo na taratibu zilizoko kwenye IPC”. Amesema Dkt. Yudas.

Aidha, Mganga Mkuu huyo alitoa vitabu vya miongozo (IPC Guidelines) kwa baadhi ya washiriki waliowakilisha vituo vyao vya kufanyia kazi ambavyo ni Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Halmashauri na Vituo vya Afya vya Jiji la Dar Es Salaam.

Kwa upande wake mratibu na mkufunzi wa mafunzo hayo Dkt. Chrisogone German amesema Shirika la Afya duniani (WHO) mwaka 2018 limetoa muongozo mpya wa kukinga na kudhibiti maambukizi (IPC Guidelines) na utaanza kutekelezwa haraka iwezekanavyo hivyo Wizara imeamua kutoa mafunzo ili kuwajengea watumishi uwezo.