Waziri Hasunga awataka mawaziri Jumuiya ya Afrika Mashariki kudumisha mshikamano

Waziri wa Kilimo nchini Tanzania Mhe. Japhet Hasunga (Mb) amesema kuwa mawaziri wenzake wa sekta ya zote ikiwemo sekta ya Kilimo kutoka nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki wanapaswa kuendeleza na kuongeza umoja na mshikamano ili kuakisi matakwa ya jumuiya katika Uzalishaji wa mazao bora ya Kilimo.
Waziri Hasunga amesema hayo Alhamisi iliyopita wakati akichangia mada kwenye mkutano wa 39 wa Baraza la mawaziri la jumuiya ya Afrika Mashariki ulioketi Jijini Arusha tangu tarehe 21-28 Novemba 2019 wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo wenyeji Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudani Kusini.
Mhe Hasunga alisema kuwa kadri ushirikiano mwema utakavyoendelezwa ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa bidii itaimarisha tija na mafanikio ya soko la mazao katika jumuiya hiyo na dunia kwa ujumla.
Aidha, amewataka watendaji wote katika nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki kutekeleza taarifa mbalimbali zinazoandikwa kwa ustadi mkubwa kwani kwa kiasi kikubwa kumekuwa na utekelezaji duni wa mipango hiyo.
Mkutano huo umefanyika katika ngazi mbalimbali ambapo Mkutano wa wataalamu ulifanyika tarehe 21-23 Novemba 2019, Mkutano wa makatibu wakuu ulifanyika tarehe 25-26 Novemba 2019, mkutano wa Mawaziri tarehe 27 -28 Novemba 2019, Kadhalika kutakuwa na Maonesho ya biashara kuanzia tarehe 28-30 Novemba 2019. Aidha mkutano wa wakuu wa nchi uliotarajiwa kufanyika tarehe 30 Novemba 2019 umeahirishwa mpaka mwezi Februari 2020.

Katika mkutano huo kwa upande wa sekta ya kilimo maswala kadhaa ya sekta ya kilimo yamejadiliwa na kufikia maazimio Katika kikao cha wataalamu na makatibu wa wakuu walioazimia kuwa nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki kupitisha mfumo wa pamoja wa kufanya tathmini ya sekta ya kilimo kwa jumuiya ya afrika mashariki (Joint Sector Review Mechanism)

Waliazimia pia kupitisha mfumo wa pamoja wa kufanya uchunguzi wa magonjwa kwa mazao ya mahindi, mpunga na maharage (Pest Risk Analysis).

Pia wameazimia pia kuanzisha mahala pa kuzalisha Viuatilifu, na kuwepo kwa miongozo ya kuhifadhi taarifa za siri za usajili wa Viuatilifu kwa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki 

Kadhalika, katika mkutano huo wataalamu walipemdekeza makatibu wakuu kuwashauri waheshimiwa Mawaziri kuagiza sekretarieti kuwezesha upatikanaji wa rasimu, mapitio na usainishaji wa makubaliano baina ya nchi mbili au zaidi juu ya udhibiti wa pamoja wa magonjwa ya wanyama yanayoweza kuvuka mipaka na kuharakisha utekelezaji wa makubaliano hayo.

Mhe Hasunga ameeleza kuwa katika mkutano huo pia wamejadili kuhusu kujiunga kwa nchi ya Congo kwenye jumuiya ya Afrika Mashariki.