Zaidi ya Tsh. Milioni 280 zatumika shule ya msingi Buhangija


Serikali kupitia Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) imetumia kiasi cha shilingi milioni 286.6 kwa ajili ya kukarabati na kujenga miundombinu katika shule ya msingi Buhangija ya Mkoani Shinyanga.

Akizungumza shuleni hapo Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Selemani Kipanya amesema mwaka 2018 Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliipatia shule hiyo fedha hizo kwa ajili ya kujenga vyumba vinne vya madarasa, mabweni mawili na matundu 18 ya vyoo.

 "Majengo haya yamesaidia sana kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na vyooni pamoja na kuboresha mazingira ya kufundushia na kujifunzia," amesema Mwalimu Kipanya.

Mwalimu Kipanya amesema shule hiyo ambayo ni jumuishi ina jumla ya wanafunzi 1,052 ambapo kati yao 230 ni wenye mahitaji maalum na kwamba wanafunzi hao wenye mahitaji maalum wanaishi bweni wakati wengine wanasoma kutwa.