Jinsi ya kuweza kupata wazo la kufanya biashara nzuri


Je nifanye biashara gani? Hilo ni moja ya swali ambalo nimekuwa nikiulizwa mara kwa mara na wajasiriamali  wakiwamo wale wanaohitaji kuanzisha aina nyingine ya biashara.
Kimsingi kuna mamilioni ya wajasiriamali ulimwenguni ambao baadhi wamebainisha kwamba vyanzo vikuu vya kupata wazo zuri la biashara ni kama ifuatavyo. 

Kitu ukipendacho sana (hobby)
Mara nyingi watu hupenda kutumia muda fulani katika siku ama wiki kujiburudisha na vitu wavipendavyo mathalani kuchezea kompyuta, kupika, muziki, safari, michezo, na kufanya  mazoezi.
Kutokana na kufanya jambo unalolipenda unaweza kuibua wazo la biashara, mathalani kuna watu wanapenda kunywa vilevi na mwisho wa siku wananzisha biashara ya baa.

Wengi wanafanya hivyo kutokana na mtandao mkubwa waliojijengea na kufanikiwa kupata wateja wengi na biashara kwenda vizuri. Kwa upande mwingine watu wanaopenda muziki huweza kubadili mapenzi hayo ya muziki na kufanya shughuli za kimuziki kibiashara.

Ujuzi na uzoefu
Tafiti nyingi zinaonyesha biashara zilizofanikiwa zimetokana na ujuzi na uzoefu wa mwanzilishi, mathalani mtu aliyeajiriwa kama mhasibu anaweza baadaye akafungua biashara ya mambo ya ukaguzi wa mahesabu, daktari anaweza kuanzisha biashara ya afya (kituo cha afya hadi hospitali) na askari anaweza kufanya biashara ya ulinzi.

Kutokana na hali hiyo tunajifunza  ujuzi na uzoefu unasaidia kuamua kuamua aina gani ya biashara ufanye.

Matumizi ya haki miliki
Kuna biashara ambazo zinafanya vizuri sokoni na kwa kuwa zimesajiliwa kisheria zinahaki miliki husika. Kwa mfano, wewe badala ya kufikiria kuanzisha biashara gani unaweza kuingia mkataba na mmiliki wa biashara hiyo ili uzalishe bidhaa ama utoe huduma kwa jina la biashara yake na kwa viwango anavyotumia ilimradi ulipie gharama ya tozo kwa kutumia hati miliki yake.

Vyombo vya habari
Vyombo vya habari ni hanzo kikubwa sana cha habari na taarifa kinachoweza kukupa wazo zuri na fursa mbalimbali za kibiashara. Vyombo vya habari vyaweza kuhusisha magazeti, runinga na siku hizi mitandao ya kijamii.

Kwa mfano unaweza kusoma au kuona habari kuhusu biashara fulani inauzwa na wewe mara moja baada ya kuiona biashara hiyo unashawishika kuinunua. Habari kwenye vyombo vya habari zinahusu mambo mengi ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiteknolojia, hivyo unapozipata ni rahisi kugundua fursa za kibiashara.

Maonyesho
Maonyesho ya kibiashara ni sehemu muhimu sana inayokutanisha wagavi, watengenezaji wa bidhaa mbalimbali, wanunuzi na wasambazaji. Kuhudhuria maonyesho ya biashara ambayo mara nyingi yanatangazwa kwenye vyombo vya habari itakusaidia   kujifunza mengi kutoka kwa watu wengine na kuvutiwa na biashara ambayo unaweza kuifanya.

Tafiti
Tafiti ni suala pana sana ila, unaweza kufanya kwa namna unavyoweza wewe, mathalani unaweza kuwa na mawazo mengi ya biashara na hujafikia uamuzi wa biashara ipi ufanye.

Kwanza unapaswa kupanga mawazo ya biashara kuendana na kipaumbele na ukibakia na mawazo matatu, jaribu kuuliza kuuliza watu mbalimbali wakiwamo wateja na watu wanaofanya biashara kama hiyo. Kwa mfano zungumza na watu wanakwenda safari ndefu kufuata bidhaa za majumbani kwa jumla, ni rahisi kwako kuanzisha biashara ili uwapunguzie adha watu wa eneo hilo.

Malalamiko
Tumia malalamiko kama njia ya kupata wazo la kuanzisha biashara mpya. Mara nyingi tumekuwa tukishuhudia foleni kubwa kwenye benki, kucheleweshewa mkopo, magari ya abiria kujaza sana na vikwazo vingine vingi, katika hili pia unaweza kupunguza malalamiko hayo kwa kuanzisha biashara mpya.

Kwa mfano, nina rafiki yangu alisajili kampuni ya kukopesha baada ya kucheleweshewa mkopo benki kwa miezi sita. Kampuni yake inatoa mkopo ndani ya muda mfupi sana ukilinganisha na benki.