Serikali yasikitishwa na mwenendo wa usajili wa vifo nchini





Na Amiri kilagalila-Njombe

Licha ya kuwepo kwa faida nyingi za usajili wa vifo nchini, lakini kumekuwepo na mwamko mdogo wa wananchi kuona umuhimu wa zoezi hilo mara baada ya kifo.
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi, idadi ya vifo nchini  vilivyosajiliwa inaonesha ni asilimia 17.5% tu ikiimaanisha vifo vingi haviandikishwi nchini.
Katika tathmini ya zoezi la usajili wa vifo katika mkoa wa Njombe lililofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya mji wa Njombe, waziri wa katiba na sheria Balozi Augustine Mahiga amesema, takwimu hizo haziridhishi na kuwataka watendaji kufanya jitihada za ziada ili kufikia malengo ya zoezi hilo.
"Takwimu hizi haziridhishi kwa hiyo tufanye jitihada za ziada ili tuweze kufikia asilimia kubwa zaidi na ninaomba mikoa mingine ipate mfano wa Njombe kwasababu katika asilimia Njombe bado mnaongoza ukilinganisha na mikoa mingine," alisema waziri Mahiga.
Mahiga aliongeza kuwa ni muhimu kuandikisha na kupata cheti cha kifo mara vinapotokea ili kuweza kupata stahiki zinazomuhusu marehemu.
"Ni muhimu sana kuhakikisha tunaandikisha tukio hilo ili kupata vyeti vya kifo ambacho kinatumika kama uthibitisho wa kisheria na hutumiwa na familia na ndugu kupata stahiki mbali mbali zinazomuhusu marehemu,Ni muhimu sana kusajili vifo mara tu vinapotokea hata kama ni vya watoto waliozaliwa na kuishi kwa dakika chache,"ameongeza.
Mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Msafiri kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Njombe amesema kwa mujibu wa takwimu zilizopo katika kanzi data ni jumla vifo 667 sawa na asilimia 20 ya vifo vinavyotarajiwa kusajiliwa kwa mwaka 2019 vimesajiliwa ndani ya miezi mitano,hivyo mkoa wa Njombe unaonesha kuimarika kwa usajili mkoani Njombe
Kaimu kabidhi wasihi mkuu ambaye ni afisa mtendaji mkuu wa wakala wa usajili wa vizazi na vifo nchini (RITA) Bi. Emmy Hudson ametoa rai kwa wananchi kuhamasika kusajili matukio ya vifo kwa faida binafsi pamoja na taifa.
“Kwa hiyo niwahamasishe wananchi kuendelea kutumia fursa hii kusajili matukio haya  kwa faida yao binafsi lakini pia kwa faida ya Taifa au serikali ili iweze kuwahudumia vizuri,” alisema Bi. Emmy Hudson