RC Kagera afanya kitu cha anina yake kuelekea kilele cha maadhimisho ya Muungano


Na: Clavery Christian Bukoba Kagera 

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti azindua rasmi maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru na miaka 57 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwaongoza wananchi , viongozi wa taasisi mbalimbali  za Serikali na zisizo za Serikali na watumishi walio chini ya taasisi hizo kufanya usafi katika soko kuu la Bukoba  na kuchangia damu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera.
Mara baada ya kushiriki usafi ndani na nje ya Soko Kuu la Bukoba Mkuu wa Mkoa Gaguti aliongea na wananchi waliokusanyika kufanya usafi pamoja naye na kuwaeleza maudhui ya  maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru na miaka 57 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwaeleza kuwa mwaka huu 2019 maadhimisho hayo yanaadhimishwa Kanda ya Ziwa ambapo mikoa miatano inashiriki kwa kufanya shughuli mbalimbali.
“Maadhimisho hayo yanaadhimishwa Kitaifa Mkoani Mwanza ambapo na mikoa ya Kanda ya Ziwa ya Kagera, Mara, Shinyanga, Simiyu na Geita inashiriki  na mkoa wetu wa Kagera sisi tumezindua rasmi maadhimisho hayo  leo kwa  kushiriki pamoja na wananchi kufanya usafi wa soko letu  pia kujitolea damu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa wahitaji ili kunusuru maisha yao,” Alifafanua Mkuu wa mkoa Gaguti.

Vilevile aliwaeleza wananchi hao kuwa wabunifu katika biashara zao ili kukuza uchumi na kipato chao lakini wakiwa wazalendo wa nchi yao, na aliwataka kila mmoja kuwa mlinzi wa nchi yake na kutumia fursa ya uwepo wa nchi jirani za Rwanda, Burundi Uganda , Congo DRC na Sudani Kusini kufanya biashara na kuufanya mkoa wa Kagera kukua zaidi kiuchumi.
Mkuu wa Mkoa Gaguti aliwaeleza wananchi hao kuwa mkoa wa Kagera unayo sababu kubwa ya  kusherehekea na kuadhimisha miaka 58 ya Uhuru na 57 ya Jamhuri mkoa umenufaika kupitia katika Sekta ya mbalimbali akitaja chache alisema kuwa tayari Serikali ya Awamu ya Tano mkoani Kagera  imejenga Vituo 14 vya Afya kwa shilingi bilioni 5.9 Hospitali tatu za Wilaya kwa gharama ya shilingi bilioni 4.5.
Sekta ya Miundombinu Meli ya MV Victoria inakarabatiwa kwa gharama ya shilingi bilioni 22.8 na mwakani 2020 mwezi Machi inaanza safari zake tena katika Ziwa Victoria kutoka Mwanza kwenda  Bandari za Bukoba na Kemondo.  Katika Sekta ya Elimu tayari Serikali imetoa  jumla ya shilingi bilioni 3.4 Kukarabati shule kongwe za Kahororo, Bukoba, Kagemu na Rugambwa na ukarabati unaendelea.
Katika hatua nyingine mkuu wa mkoa Gaguti aliwaongoza wananchi na viongozi mbalimbali kuchangia  damu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera ambapo mpaka anaondoka katika eneo hilo tayari chupa 63 zenye ujazo wa nusu lita za damu zilikuwa zimekusanywa malengo yakiwa ni kukusanya chupa 400 kwa siku hiyo tu.
Kilele cha Maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru na 57 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni tarehe 9 Desemba 2019 Mkoani Mwanza na Kaulimbiu ya Maadhimisho hayo ni “Miaka 58 ya uhuru na miaka 57 ya Jamhuri: Uzalendo, Uwajibikajina Ubunifu ni Msingi wa Ujenzi wa Uchumi na Taifa letu.”