Bibi harusi feki ashtakiwa Uganda


Mwanaume wa kiganda anayeshutumiwa kwa kujifanya mwanamke kabla ya kuolewa na imam ameshitakiwa kwa makosa yasiyo ya kawaida pamoja na wizi, gazeti la Daily Monitor limeripoti .

Richard Tumushabe aligundulika jinsia yake mara baada ya kukamatwa na polisi kwa shutuma za wizi wa televisheni na nguo za jirani yake.

Imam aliyemuoa mwanaume mwenzake akidhani ni mwanamke alifutwa kazi na baraza kuu la Waislamu Uganda.

Sheikh asimamishwa kazi kwa 'kumuoa' mwanaume
Je ni kwa nini Uganda inawakamata na kuwashtaki wapenzi wa Jinsia moja?
Huku mjadala kuhusu kama kweli alifahamu jinsia ya bi harusi wake wiki mbili zilizopita alipofanya nikka naye, baraza hilo linasisitiza kuwa kuna dosari kubwa kwa upande wa imam huyo na hastahili kuendelea na kazi yake.


Awali taarifa zilisema kuwa Sheikh Mohammed Mutumba anadai kuwa alipata mshtuko wiki mbili baada ya kugundua kuwa mke aliyemuoa aliyekuwa akivalia vazi la hijab kila wakati na anafahamika kama Swabullah Nabukeera alikuwa ni mwanaume anayeitwa Richard Tumushabe.

Ukweli kuhusu jinsia yake ulibainika baada ya polisi kumkamata Tumushabe kwa madai ya wizi wa televisheni na nguo za jirani yake.

"Wakati polisi wakifanya shughuli zao za kila siku, askari wa kike alimkagua sehemu zake za mwili kabla hajampeleka jela. Na kuwashangaza maafisa wa polisi kuwa mtuhumiwa huyo kuwa aliweka nguo katika sidiria ili aonekane ana matiti,"bwana Mugera alinukuliwa.

Sheikh Mutumba - ambaye ni imamu wa msikiti uliopo kijiji cha Kyampisi, kilomita takribani 100 (62 miles) kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Uganda, Kampala - alidai kuwa hajafanya naye tendo la ndoa mke wake huyo tangu amuoe kwa sababu alisema kuwa alikuwa ana matatizo ya kiafya yaliyomfanya kuendelea kupata hedhi na ilimbidi amvumilie mpenzi wake.

"Tayari tumemshtaki kwa kosa la kujiigiza kuwa mtu mwingine,vilevile kwa kosa la wizi na kujipatia vitu kwa ulaghai ," bwana Mugera alisema.

Gazeti la Daily Monitor limeripoti kuwa Sheikh Abdul Noor Kakande, ambaye ni kadhi wa ukanda huo (jaji wa kiislamu), amesema kuwa tukio hilo ni la kushangaza sana na halikubaliki, hivyo imam anafanyiwa uchunguzi.

Vilevile Baraza kuu la Sheikh mkuu wa msikiti ambao sheikh Mutumba anaswalia, Isa Busuulwa, amesema kuwa amemsimamisha kazi sheikh huyo kwa heshima ya imani ya kiislamu hivyo hatoruhusiwa kuswalisha katika msikiti wowote ule.

Baadhi ya wanawake nchini Uganda na wao wametowa hisia zao wakisema Imamu huyo kuna kitu anaficha:

"Haiingii akilini kwa namna moja au nyingine, hata kama ni mtu wa kujifunika na tunaelewa waislamu wanajifunika sana.Lakini hawa watu walifahamiana na kupelekana nyumbani ,na kwa muda wa wiki mbili kuna mambo mengi kati ya mume na mke, kuna kuoga,kubadilisha nguo, kuangaliana na mambo mengine mengi."

Mapenzi ya watu wa jinsia moja iliharamishwa nchini Uganda chini ya sheria za ukoloni katika kifungu kinachokataza mtu kufanya ngono kinyume na kawaida.

Vilevile shughuli zote za wapenzi wa jinsia moja ni haramu na kinyume na tamaduni za watu wa Uganda.

Kwa sheria za sasa hivi ambazo ni za kutoka enzi za utawala wa waingereza, mapenzi ya jinsia moja ni kosa ambalo watu wanaweza kupewa adhabu ya kifungo cha maisha na wanaharakati wanasema sheria hii mpya itaanzisha mashambulizi makali kwa watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Uganda yapanga kunyonga wapenzi wa jinsia moja
Mwezi Oktoba, 2019, Waziri wa maadili nchini Uganda alitangaza mipango wa kuanzisha tena sheria inayopinga mahusiano ya jinsia moja, iliyofutwa na mahakama ya kikatiba mwaka 2014.

Waziri Simon Lokodo ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa sheria hiyo mpya itamuadhibu hukumu ya kifo yeyote atakayeenda kinyume nayo.

''Sheria yetu ya sasa inatubana sana. Inasema kuwa kitendo hiki ni jambo la kuvunja sheria. Tunataka iwekwe wazi kuwa mtu yeyote anaepigia debe suala hili anaweza kushtakiwa.

Wale wanaofanya vitendo vya kushangaza watahukumiwa kifo.''

Aliendelea kueleza kuwa, ''mahusiano ya aina hii sio kitu cha kawaida kwa watu wa Uganda na kumekuwa na waajiriwa wengi shuleni ambao ni wapenzi wa jinsia moja wanaowafundisha watu uongo kuwa mtu anazaliwa na hisia za mapenzi ya jinsia moja.''

Mwezi Februari mwaka 2014, Rais Yoweri Museveni alisaini muswada wa sheria wa kuwabana wapenzi wa jinsia moja lakini sheria hiyo ilifutwa na mahakama mwezi Agosti mwaka huo huo.

Mabadiliko hayo yalitokea baada ya kubainika kuwa wabunge walipitisha sheria hiyo bila kufuata utaratibu wa kisheria.